Waziri wa Habari wa Zambia akutana na Balozi wa China nchini humo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 26, 2022

LUSAKA - Waziri wa Habari wa Zambia Chushi Kasanda amekutana na Balozi wa China nchini Zambia Li Jie kwa njia ya mtandao Jumatatu ya wiki hii, ambapo wamebadilishana mawazo kuhusu uhusiano wa Zambia na China na ushirikiano wa kivitendo baina ya nchi hizo mbili.

Katika mkutano huo, Kasanda amesema kuwa China imefanya jukumu kubwa katika mapambano ya kimataifa dhidi ya janga la UVIKO-19, na kuwa mfano wa kuigwa kwa Dunia.

Wizara ya Habari ya Zambia ilisema katika taarifa yake ya Jumanne wiki hii kwamba, Waziri Kasanda amesema Zambia inapenda kujifunza uzoefu wa hali ya juu wa China katika ujenzi wa vyombo vya habari na kuendelea kuwasiliana na China kuhusu masuala yanayofuatiliwa na pande hizo mbili, akitumai kuwa China inaweza kutoa msaada zaidi kwa Zambia.

Waziri huyo pia alirejea kumbukumbu ya China kuhusu kuunga mkono Zambia wakati wa harakati za kupigania uhuru.

"Wananchi wa Zambia watakumbuka daima vitendo vya Wachina kwa kutoa msaada kwa Zambia wa kujenga TAZARA (Reli) wakati China yenyewe ilikuwa ikikabiliwa na changamoto za kiuchumi na pia wakati Zambia haikuwa na njia ya uhakika ya kuunganishwa na bahari kwa ajili ya kuagiza na kuuza bidhaa nje. Uungwaji mkono kama huo usio na kikomo unaonesha kwamba China ni rafiki wa Zambia wa nyakati zote," amesema.

Pia amepongeza ushirikiano kati ya Zambia na China katika jukwaa la kimataifa.

Kwa upande wake, Balozi Li amesema kuwa urafiki wa "nyakati zote" kati ya China na Zambia unapata matokeo ya manufaa ya ushirikiano wa vitendo. Ameongeza kwamba, Zambia ni mojawapo ya nchi zinazofaidika na maendeleo ya China. Na kwamba, China inapenda kuimarisha ushirikiano na Zambia katika utengenezaji wa filamu na vipindi vya televisheni, kuwajengea uwezo wafanyakazi wa vyombo vya habari, na ujenzi wa miundombinu ya habari chini ya mfumo wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) na Pendekezo la Ukanda Mmoja na Njia Moja.

Li alieleza matumaini yake kuwa Zambia inaweza kuandaa sera zenye manufaa zaidi za kuvutia biashara na uwekezaji, na kujenga mazingira mazuri kwa uwekezaji wa China. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha