Kamati ya Olimpiki ya Beijing 2022 yasema China haidanganyi kamwe majibu ya vipimo vya UVIKO-19

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 30, 2022

Picha iliyopigwa Januari 10, 2022 ikionesha vifaa vya kudhibiti janga la UVIKO-19 katika Kituo Kikuu cha Vyombo vya Habari kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki na Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Majira ya Baridi ya Mwaka 2022 huko Beijing. (Xinhua/Xu Zijian)

BEIJING - Huang Chun, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Kuzuia na Kudhibiti Janga la Virusi vya Korona ya Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022 amesema kwamba, haina haja ya kudanganya matokeo ya vipimo vya UVIKO-19, na China kamwe haitafanya hivyo.

 

Akizungumzia habari zilizochapishwa na vyombo vya habari vya nchi za nje kuhusu uwezekano wa China kuchakachua matokeo ya vipimo vya virusi vya korona ili kuwaathiri wanamichezo, Huang ameuhakikishia mkutano na waandishi wa habari Jumamosi wiki hii kwamba majibu ya vipimo ni ya kweli.

Ndani ya eneo lililofungwa kitanzi, vipimo vyote vya UVIKO-19 ni vipimo vya PCR, ambavyo vinatambuliwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) pamoja na wataalam wa matibabu kutoka ndani na nje ya China.

"Kwa upimaji (virusi vya korona), tulichagua maabara zenye sifa. Zimetambuliwa na mamlaka ya afya ya umma nchini China. Zikiwa na vifaa vilivyoidhinishwa, zinafuata taratibu za kawaida na kali katika upimaji na zina mfumo kamili wa usimamizi ili kuhakikisha ubora na usalama. Wahudumu wa afya katika uchukuaji sampuli na upimaji, wote wenye taaluma, wamepitia mafunzo kabla ya kufanya kazi zao," amesema.

Huang ameongeza kuwa mamlaka husika za Serikali ya China mara nyingi hutembelea maabara hizo ili kukagua ubora wao pamoja na usalama, na matokeo chanya ya maambukizi ya UVIKO-19 yatathibitishwa tu baada ya kupimwa mara ya pili.

Dk Brian McCloskey, Mwenyekiti wa Jopo la Wataalamu wa Kimatibabu la Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022, pia amethibitisha kuwa vipimo vya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022 viko katika viwango vya kimataifa na vinafuata miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

"Nataka wanamichezo na washikadau wote wawe na uhakika. Hakuna haja ya kushuku sana uaminifu wa mifumo yetu," Huang ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha