Ujumbe muhimu kutoka shughuli nyingi za kidiplomasia za Rais Xi Jinping kwenye Michezo ya Olimpiki

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 08, 2022

Rais Xi Jinping wa China akitoa hotuba kwenye hafla ya kuwakaribisha wageni mashuhuri kutoka duniani kote waliohudhuria sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022 mjini Beijing, Mji Mkuu wa China, Februari 5, 2022. (Xinhua/Zhai Jianlan)

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping ameshiriki katika mikutano ya ana kwa ana ya ngazi ya juu na viongozi wa kigeni waliofanya ziara mjini Beijing kwa ajili ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing licha ya changamoto zinazosababishwa na janga la UVIKO-19.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Xi alifanya mikutano ya pande mbili na wakuu wa nchi wapatao 20 pamoja na viongozi wa serikali na mashirika ya kimataifa, na kufanya hafla ya kuwakaribisha wageni hao.

Yafuatayo ni mambo muhimu yaliyochukua nafasi kubwa kwenye mikutano hiyo kati ya Rais Xi Jinping na viongozi hao:

Mshikamano

Miongoni mwa viongozi waliozuru China ni Rais wa Russia Vladimir Putin, Waziri Mkuu wa Pakistani Imran Khan, viongozi wa nchi za Asia ya Kati ambao walikutana na Xi wakati wa mkutano wa kilele uliofanyika siku chache kabla ya Michezo hiyo, na Rais wa Serbia Aleksandar Vucic.

Umoja, mshikamano na kuwa pamoja ndiyo maneno muhimu yaliyojadiliwa zaidi wakati wa mikutano hiyo.

"Tutahimiza moyo wa Harakati za Olimpiki na kukabiliana na changamoto zinazoikabili jumuiya ya kimataifa kwa kupitia mshikamano," amesema Xi na kuongeza kuwa njia pekee ya nchi zote kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa ufanisi ni kuimarisha mshikamano na ushirikiano na kufanya kazi kwa ajili ya mustakabali wa pamoja wa baadaye.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Dunia sasa inahitaji michuano ya Olimpiki ya Majira ya baridi yenye mafanikio ili kutuma ujumbe wa wazi kwamba watu wa nchi, kabila na dini mbalimbali wanaweza kuondokana na tofauti ili kufikia mshikamano na ushirikiano.

Maendeleo

Kuhimiza maendeleo madhubuti ni suala lingine nyeti kwenye mikutano kati ya Rais Xi na viongozi hao.

Licha ya miradi muhimu kati ya nchi mbili kuanzia nishati hadi uchumi wa kidijitali, ushirikiano wa Pendekezo la Ukanda Mmoja na Njia Moja ulijadiliwa sana.

Miradi mikuu ya miundombinu kama vile reli ya Hungary-Serbia na reli ya China-Kyrgyzstan-Uzbekistan ilipata msukumo. Rais wa Kyrgyzstan Sadyr Zhaparov amesema kuwa nchi hiyo inapenda kushirikiana na China kwa karibu ili kuifanya reli ya China-Kyrgyzstan-Uzbekistan kuwa mradi kinara katika ushirikiano wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja".

Argentina pia imetia saini Mkataba wa Maelewano na China kuhusu ushirikiano wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja".

Viongozi wengi pia waliunga mkono Pendekezo la Maendeleo ya Dunia (GDI) lililopendekezwa na Rais Xi mwaka jana, ambalo linachukuliwa kuwa la muhimu katika kufufua uchumi na kuhimiza maendeleo endelevu.

Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev amesema Kazakhstan itaendelea kuunga mkono kikamilifu na kushiriki katika ushirikiano chini ya Pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja" huku ikiunga mkono GDI iliyopendekezwa na Rais Xi.

Kuheshimiana

Katika mkutano na Guterres, Rais Xi alisema kuwa hakuna mfumo wa utawala unaopaswa kuzingatiwa kama pekee wa kufuata, wala hakuna mfumo mmoja wa maendeleo unaofaa nchi zote.

Kama ilivyokubaliwa na China na Russia, nchi mbili ambazo zimejenga mfano wa kuigwa wa uhusiano wa kimataifa katika Karne ya 21, watu wa nchi zote wana haki ya kuchagua aina na njia za kutekeleza demokrasia zinazoendana na hali zao za kitaifa.

"Tunapaswa kushikiria kuheshimiana, kutendeana kwa usawa, kufanya mazungumzo na mashauriano, kujitahidi kuondokana tofauti na migogoro, na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya Dunia yenye amani ya kudumu," Xi alisema wakati wa hafla ya kukaribisha viongozi hao iliyofanyika Jumamosi ya wiki iliyopita. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha