China yaidhinisha maeneo zaidi ya majaribio ya biashara ya kimataifa ya mtandaoni

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 09, 2022

Picha iliyopigwa Agosti 20, 2021 ikionesha eneo la maonesho ya biashara ya kimataifa ya mtandaoni na uchumi wa kidijitali katika Maonesho ya tano ya China na nchi za Kiarabu huko Yinchuan, Mkoa unaojiendesha wa Ningxia, Kaskazini-Magharibi mwa China. (Xinhua/Wang Peng)

BEIJING - Baraza la Serikali la China limeidhinisha maeneo zaidi ya majaribio ya biashara ya kimataifa ya mtandaoni katika miji na sehemu 27 huku serikali ikijaribu kuleta utulivu kwenye biashara ya nje na uwekezaji wa kigeni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza la Serikali, maeneo mapya ya majaribio, ikiwa ni pamoja na yale ya Erdos katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani na Mji wa Yangzhou katika Mkoa wa Jiangsu, yataiga na kuendeleza uzoefu uliopatikana kutoka kwa makundi matano ya awali ya maeneo ya majaribio.

Huku likijaribu kukuza maendeleo ya kiwango cha juu ya biashara, Baraza la serikali pia limesisitiza juhudi za kuhakikisha usalama wa taifa, usalama wa mtandao, usalama wa data, na usalama wa kibaiolojia ili kukuza mazingira ya kibiashara yanayofaa kwa wadau wa soko.

Biashara ya kimataifa ya mtandaoni ya China imekuwa ikipanuka kwa kasi zaidi kuliko biashara ya nje kwa ujumla, na mchango wake katika biashara ya nje kwa ujumla umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Tangu Mwaka 2015, Baraza la Serikali la China limeanzisha maeneo 105 ya majaribio ya biashara ya kimataifa ya mtandaoni kwa makundi matano. Mtindo mpya huo wa biashara umekuwa muhimu katika kuongeza ukuaji wa biashara ya nje ya China.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa jumla ya biashara ya bidhaa kwa China iliongezeka kwa kiwango kikubwa Mwaka 2021, ikizidi dola trilioni 6 za kimarekani kwa mara ya kwanza, licha ya janga la UVIKO-19 kuendelea kuathiri biashara ya kimataifa.  

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha