IOC yasifu “Matumizi mara Mbili ya Viwanja vya Michezo ya Olimpiki”: Kujumuisha sifa bora za Olimpiki Endelevu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 10, 2022

Katika mkutano na waandishi wa habari wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing Februari 9, Msimamizi mkuu wa Chapa na Maendeleo Endelevu wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa IOC Marie Sallois alisifu “Matumizi ya mara mbili ya viwanja vya michezo ya Olimpiki” ya Beijing, akiamini kwamba njia hiyo ya kutumia viwanja inaleta pamoja uzoefu wa Michezo ya Olimpiki iliyopita na faida endelevu.

Kutumia viwanja vya michezo baada ya michezo mikubwa kumalizika kumekuwa ni tatizo la kidunia. Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing inatumia viwanja vingi vya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Joto ya Beijing 2008, ikiwemo Uwanja wa Taifa, Jumba la Michezo la Taifa, Kituo cha Michezo ya Kuogelea cha Taifa, Kituo cha Michezo cha Wukesong, Jumba la Michezo la Mji Mkuu n.k., ambavyo vimebadilika kuwa vituo vya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi kutoka Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Joto.

Sallois anaamini kuwa, njia hiyo ya kutumia viwanja vya michezo inatoa mfano wa kuigwa kwa Michezo ya Olimpiki ijayo, na pia kutoa mpango endelevu wa kuendesha viwanja. “Viwanja vyote vya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi vina matumizi mbalimbali. Vinaweza kutumika kwa mashindano ya michezo, kufanya mazoezi, kufanya shughuli za kitamaduni, hata baadhi yake vinaweza kutumika wakati wa majira ya joto pia majira ya baridi. Matumizi ya viwanja hivyo vya michezo yanalenga makundi ya watu tofauti na hujumuisha shughuli mbalimbali. Ninaamini yatatumiwa kwa muda mrefu.”

Alihitimisha kwa kusema kuwa, mfumo wa kutumia viwanja vya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing umejumuisha sifa bora za Michezo ya Olimpiki iliyopita kwa upande wa uendelevu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha