Waandaaji wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing wasema wamejitayarisha vema kukabiliana na hali mbaya ya hewa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 11, 2022

BEIJING - Huku theluji na kushuka kwa hali ya joto kukitarajiwa mjini Beijing na Zhangjiakou wikendi hii, Kamati ya Maandalizi ya Olimpiki ya Beijing 2022 (BOCOG) imesema kuwa inachukua hatua nyingi za kuhakikisha uendeshaji mzuri wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi inayoendelea, na afya na usalama wa wahusika wote licha ya hali mbaya ya hewa.

"Tunapaswa kuheshimu asili na kuhakikisha mashindano yaliyopangwa ya Michezo yanafanyika, lakini wakati huo huo tutahakikisha usalama na afya ya wanamichezo, wafanyakazi na watu wa kujitolea," Zhao Weidong, Msemaji wa BOCOG amesema Jumatano wiki hii.

Amesema kwamba, ili kujiandaa vema kwa hali mbaya ya hewa, BOCOG itafanya kazi kwa kuzingatia utabiri sahihi zaidi wa hali ya hewa.

"Watabiri wa hali ya hewa watawapa takwimu za hali ya hewa wataalam wa kiufundi kutoka Shirikisho la Kimataifa (IFs), ambao wataamua kama inahitaji kubadili ratiba ya baadhi ya mashindano ya michezo, na namna gani ya kutekeleza hilo” amesema Zhao.

"Kwa ujumla, theluji haitaathiri ratiba. Iwapo kutakuwa na hali mbaya ya hewa tutaratibu na IOC (Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki), IFs na OBS (Huduma za Utangazaji wa Olimpiki)."ameongeza.

“Wakati huo huo, majumba na viwanja vya Michezo pia vimejiandaa kuondoa theluji na barafu, kuwa na vifaa vya kujikinga na kuzuia kuteleza kwenye barafu. Ningependa kuwakumbusha waandishi wa habari kuvaa nguo za kujikinga dhidi ya baridi," Zhao amesisitiza.

Naye Huang Chun, Naibu Mkurugenzi wa ofisi ya kukabiliana na mlipuko wa virusi vya korona ya BOCOG amesema, ili kuhakikisha kwamba wanamichezo waliojeruhiwa wanapata matibabu haraka iwezekanavyo wakati wa Michezo, BOCOG imeanzisha timu ya matibabu ya kitaalamu na ya kiwango cha juu

Kwa mujibu wa Huang, watoaji huduma za matibabu wote wanatoka hospitali kuu za Beijing na Mkoa wa Hebei, wakati vifaa na taratibu za matibabu zote zimeidhinishwa na IOC. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha