Mji Mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa wazindua jengo maarufu lililojengwa na China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 15, 2022

Ethiopia siku ya Jumapili ya wiki iliyopita imezindua jengo maarufu lenye urefu wa Mita 209.15 lililoko katikati ya mji mkuu wake Addis Ababa, ambalo linamilikiwa na Benki ya Kibiashara ya Ethipia (CBE).

Makao makuu mapya ya Benki ya Kibiashara ya Ethiopia (CBE) yamejengwa na Kampuni kubwa ya ujenzi ya China, State Construction Engineering Corporation (CSCEC).

Tukio la uzinduzi wa jengo hilo liliambatana na maadhimisho ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa CBE na lilihudhuriwa na maafisa wakuu wa Serikali ya Ethiopia, wanadiplomasia wa China nchini humo, na wawakilishi wa CBE na CSCEC.

Akiutaja uzinduzi wa jengo hilo kuwa hatua muhimu, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema, "Nimefurahi sana tunapokusanyika hapa leo kuzindua jengo hili zuri huku pia tukiadhimisha miaka 80 ya benki hii yenye historia ya muda mrefu."

Ahmed amesema, CBE inaakisi kujitolea kwa miaka mingi kwa Ethiopia na matarajio ya kuanzisha na kuendeleza taasisi za kisasa, huku akisisitiza haja ya kuifanya sekta ya benki kuwa ya kisasa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Mradi wa jengo hilo, unaohusisha ujenzi wa jukwaa mbili za ghorofa tano na jengo kuu, umepata sifa kubwa miongoni mwa wataalam wa Ethiopia. Linatajwa kuwa jengo refu zaidi katika eneo la Afrika Mashariki.

Rais wa CBE Abie Sano amesema mradi huo umetumika kama njia kwa wanafunzi wa uhandisi wa Ethiopia na kampuni za ujenzi za nchi hiyo kujifunza teknolojia ya kiwango cha juu.

Akibainisha kuwa vifaa vya ujenzi na teknolojia zilizotumika katika mchakato wa ujenzi zinakidhi viwango vya kimataifa, ameongeza, "Juhudi za kujifunza wakati wa kukaa kwetu na wataalam wenzetu kutoka China imekuwa hatua nyingine muhimu."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha