Chapa ya Uswisi ya Stockli yaona Michezo ya Olimpiki ya Beijing kama kichocheo cha biashara yake nchini China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 17, 2022

GENEVA – Kampuni ya vifaa vya Michezo ya Uswisi Stockli ambayo ni mtengenezaji mkuu wa vifaa vya michezo ya kuteleza kwenye theluji imesema Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 imeongeza nguvu mpya katika biashara yake nchini China na kwamba inatarajia kuona ukuaji wa biashara yake kwa tarakimu mbili katika miaka michache ijayo.

"Tunaamini kwamba hata baada ya Olimpiki, mwelekeo wa ukuaji wa michezo ya majira ya baridi nchini China utaendelea," Christian Gut, Afisa Mkuu wa mauzo na masoko katika Kampuni hiyo ya Stockli ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano yaliyofanyika kwa njia ya mtandao.

"China ina uwezo wa kuwa moja ya soko kubwa zaidi duniani katika miaka ijayo. Ni soko muhimu sana kwetu."

Ikiwa na historia ya toka Mwaka 1935, kampuni hiyo inayomilikiwa na familia moja inauza vifaa vya michezo ya kuteleza kwenye theluji katika nchi 30 na kuajiri watu 100.

Gut amesema kuwa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022 imeleta msukumo mkubwa kwa biashara yake.

"Katika miaka ya hivi karibuni, tumeona uwekezaji mkubwa katika soko la China, na maeneo ya kuteleza kwenye theluji ya nchi hiyo." amesema.

Gut anatarajia watelezaji wengi wa kwenye theluji kutoka China watasafiri kwenda kwenye milima ya Uswisi kuteleza kwenye theluji mara tu vizuizi vinavyohusiana na janga la UVIKO-19 vitakapoondolewa.

"Kwa mujibu wa taarifa zetu, nusu ya watu wanaoshiriki kwenye mchezo wa kuteleza kwenye theluji hutembelea nje ya nchi. Hii ina ushawishi mzuri sana na pia ni sababu inayotufanya tuwepo kwenye mitandao ya kijamii ya China kama kampuni ndogo ya Uswisi."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha