Watu maarufu duniani, wanamichezo wasema Michezo ya Olimpiki ya Beijing imeonesha moyo wa michezo na mshikamano

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 21, 2022

BEIJING - Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 imewavutia sana maafisa, wasomi na wanamichezo kutoka kote duniani, ambao wamesema moyo wa michezo na mshikamano uliooneshwa wakati wa michezo hiyo umetoa matumaini mengi kwa jumuiya ya kimataifa.

Mchezaji nyota wa Bosnia na Herzegovina Mirza Nikolajev alipata umaarufu miongoni mwa Wachina wengi baada ya sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing, kufutia video na picha zake zinazomwonesha akikonyeza macho yake mbele ya kamera wakati wa gwaride la wanamichezo kusambaa.

Katika Kijiji cha Olimpiki, "kila mtu siku zote alikuwa mchangamfu na akitabasamu wakati wote. Walifanya kila wawezalo kukufanya ujisikie uko nyumbani," Nikolajev amesema katika mahojiano kwa njia ya video.

"Nina furaha sana kwamba nilipata nafasi ya kuwakilisha nchi yangu. Siyo kwa jinsi nilivyotarajia, lakini bado hii ilikuwa uzoefu wa kushangaza," ameongeza.

Wanamichezo wengi wameeleza kwamba, hatua za kuzuia na kudhibiti janga la UVIKO-19 katika Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing ni za kisayansi sana, ambazo zinahakikisha wanamichezo wanaweza kufanya mazoezi na kushindana katika mazingira salama.

Mchezaji mkongwe wa Romania, Raluca Stramaturaru, ambaye alishindana katika mbio za kupokezana za timu ya luge kwenye michezo hiyo ya mwaka huu, amesema kuwa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 ndiyo Olimpiki bora zaidi ambayo amewahi kushiriki.

Martin Begino, mkuu wa ujumbe wa Argentina kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022, alipongeza maandalizi na mpangilio wa Michezo hiyo, akisema kuwa michezo hiyo imeandaliwa kwa utaratibu bora.

Kama inavyoonekana kutokana na miundombinu kamili ya michezo hiyo, China imetilia maanani sana maandalizi na mpangilio wa Michezo hiyo, alisema Begino, akiongeza kuwa kamati ya maandalizi inaweza kusikiliza kwa subira maoni ya wajumbe mbalimbali na kutatua matatizo kwa wakati.

Michezo ya 24 ya Olimpiki ya Majira ya baridi inastahili kusifiwa zaidi, alisema Yevgeny Zaitsev, Mkuu wa Kituo cha Masomo ya Russia na China katika Chuo Kikuu cha Moscow cha Lomonosov cha Russia.

Zaitsev aliliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano kuwa, licha ya ugumu unaosababishwa na janga la UVIKO-19, China imetimiza ahadi yake kwa kiwango kikubwa na imewasilisha Olimpiki ya Majira ya baridi, iliyo rafiki kwa mazingira, jumuishi, wazi na safi.

Zaitsev amesema kauli mbiu ya Michezo ya Olimpiki ya "Haraka Zaidi, Juu Zaidi, Nguvu Zaidi - Pamoja," ilitafsiriwa vema zaidi kwenye michezo hiyo ya Beijing 2022, na moyo wa michezo wa wanamichezo ambao walishinda changamoto mbalimbali na kushiriki na kushinda katika michezo hiyo umetia moyo Dunia.

Kimmo Suomi, profesa wa mipango ya michezo katika Chuo Kikuu cha Jyvaskyla cha Finland, pia alipongeza Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing.

Suomi ameliambia Xinhua katika mahojiano kwamba, sherehe ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing ilikuwa ya kuvutia na ilitoa ujumbe wa matumaini kwa Dunia kwamba wakati Dunia inakumbwa na changamoto zinazosababishwa na janga hilo, mtu anaweza pia kuishi maisha ya kawaida katika Olimpiki.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha