China yapata mafanikio ya kusisimua Kwenye Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi ya Beijing 2022

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 21, 2022

Gao Tingyu, mbeba bendera wa Ujumbe wa Olimpiki wa Timu ya Jamhuri ya Watu wa China, akitembea kuongoza wenzake wakati wa sherehe za kufunga Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 kwenye Uwanja wa Michezo wa Taifa, Februari 20, 2022. (Xinhua/Ju Huanzong)

BEIJING - China imejinyakulia medali tisa za dhahabu na medali 15 kwa jumla katika Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022, idadi ambayo imeweka rekodi ya juu kwa Timu ya China kushinda medali nyingi zaidi katika Olimpiki moja ya Majira ya Baridi.

Zaidi ya ubora katika michezo hiyo, China, nchi mwenyeji imepata msukumo mkubwa katika nyanja tofauti.

Ikiwa na ujumbe wa Timu yenye washiriki 388, wakiwemo wanamichezo 177 walioshindana katika mashindano tofauti 104 ya aina 15 katika michezo saba, China ililenga kupata matokeo bora zaidi katika Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022.

Michezo ya kwenye theluji ilikuwa sehemu dhaifu kwa China hapo awali, ikichangia medali moja tu ya dhahabu kati ya medali 13 kabla ya Michezo hiyo ya Beijing, ambayo ilitokana na mafanikio ya Mchezaji Han Xiaopeng katika mchezo wa kuteleza kwenye theluji na kuruka hewani kwa mtindo huru kwa wanaume huko Turin 2006.

Lakini hali imebadilika wakati huu, kwani China imeshinda medali tano kati ya tisa za dhahabu katika michezo ya kwenye theluji.

Gu Ailing akishiriki fainali ya mchezo wa kuteleza kwenye theluji na kuruka hewani kwa mtindo huru kwenye nusu pipa kwa wanawake kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 katika Bustani ya Theluji ya Genting huko Zhangjiakou, Mkoa wa Hebei Kaskazini mwa China, Februari 18, 2022. (Xinhua/Hu Huhu)

Kuibuka kwa wachezaji vijana wenye kusisimua Gu Ailing na Su Yiming, kumeifanya Timu ya China ipate msukumo mkubwa katika michezo hiyo ya kwenye theluji.

Gu alianza kwa kushinda medali ya kwanza ya dhahabu kwa Timu ya China kwa wanawake kwenye mchezo wa kuteleza kwenye theluji na kuruka hewani kwenye jukwaa kubwa, aliongeza medali ya fedha kwenye mchezo wa kuteleza kwenye theluji kwenye mteremko mkali na kuruka hewani kwa ubao, na baadaye kushinda medali ya dhahabu katika mchezo wa kuteleza kwenye theluji kwenye nusu pipa.

Akiwa na umri wa miaka 18 na siku 168, Gu ndiye mwanamichezo mwenye umri mdogo zaidi kushinda medali tatu za kibinafsi kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi. Pia anakuwa mwanamichezo wa kwanza wa mchezo wa kuteleza kwenye theluji na kuruka hewani kwa mtindo huru kushinda medali tatu kwenye Olimpiki moja ya Majira ya baridi.

"Imekuwa wiki mbili mfululizo za hali ya juu na chini ambayo nimewahi kuwa nayo maishani mwangu. Imebadilisha maisha yangu milele," amesema Gu.

Su Yiming mshindi wa medali ya dhahabu katika mchezo wa kuteleza kwenye theluji kwa ubao na kuruka hewani akisherehekea ushindi wake kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022, Februari 15, 2022. (Xinhua/Huang Zongzhi)

Mchezaji mwingine wa Timu ya China aliyeng’ara katika michezo ya kwenye theluji ni Su Yiming, ambaye alitimiza umri wa miaka 18 siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita. Su alishinda medali ya fedha kwenye mchezo wa kuteleza kwenye theluji kwenye mteremko mkali na baadaye alishinda medali ya dhahabu katika mchezo wa kuteleza kwenye theluji na kuruka hewani kwenye jukwaa kubwa.

Xu Mengtao akishiriki fainali ya mchezo wa kuteleza kwenye theluji na kuruka hewani kwa mtindo huru kwa wanawake kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 iliyofanyika Bustani ya Theluji ya Genting, Februari 14, 2022. (Xinhua/Xue Yubin)

Wanamichezo wengine wa China walioshinda medali ni Xu Mengtao na Qi Guangpu, waliotwaa medali ya dhahabu katika mchezo wa kuteleza kwenye theluji na kuruka hewani kwa wanaume na wanawake na baadaye walipata medali ya fedha pamoja na Jia Zongyang katika timu ya jinsia mchanganyiko.

Fan Kexin (Wa kwanza Kushoto) akiongoza wakati wa fainali ya mbio za kupokezana za njia fupi za kuteleza kwa kasi kwenye barafu kwenye Uwanja wa ndani wa Beijing, Februari 5, 2022. (Xinhua/Lan Hongguang)

Katika mbio za njia fupi za kuteleza kwa kasi kwenye barafu Timu ya China ikiwa na wachezaji Fan Kexin, Qu Chunyu, Ren Ziwei na Wu Dajing walipata ushindi wa medali ya dhahabu kwenye mbio za kupokezana za njia fupi za kuteleza kwa kasi za mita 2,000. Baadaye katika mbio za mita 1,000 Ren Ziwei alinyakua medali yake ya kwanza ya dhahabu na kufuatiwa na Li Wenlong aliyepata medali ya fedha. Timu ya China pia ilishinda medali ya shaba katika mbio za kupokezana za mita 3,000 kwa wanawake.

Mwanamchezo Gao Tingyu amepata medali ya dhahabu katika mbio za mita 500 za kuteleza kwenye barafu kwa wanaume, akiwa bingwa wa kwanza wa Olimpiki kwa mwanaume katika mbio za kuteleza kwenye barafu.

Sui Wenjing (Kulia) na Han Cong wakitumbuiza wakati wa shindano la kucheza na kuteleza kwenye barafu, kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya bairidi ya Beijing 2022, Februari 19, 2022. (Xinhua/Lan Hongguang)

Wachezaji wengine wa China na medali walizoshinda zikiwa kwenye mabano ni Sui Wenjing na Han Cong (dhahabu), Yan Wengang (shaba)

Kando na kushinda medali, China imeshuhudia mafanikio mengi katika historia ya Olimpiki, ikiwa ni pamoja na kushiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano 35 kati ya 104 ambayo wanamichezo wa China walishiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha