

Lugha Nyingine
China yapanga majukumu ya kuendeleza ustawishaji wa vijijini Mwaka 2022
Wakulima wakivuna pilipili hoho katika wilaya ya Jiaji, mji wa Qionghai, Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China, Februari. 10, 2022. (Picha na Meng Zhongde/Xinhua)
BEIJING - China imetangaza "waraka namba 1 wa serikali kuu" kwa Mwaka 2022 unaoelezea majukumu muhimu ya kusukuma mbele ustawishaji wa vijijini mwaka huu.
Ikiwa waraka wa kwanza wa sera unaotolewa na Serikali Kuu ya China kila mwaka, waraka huo uliotolewa Jumanne wiki hii ni kiashirio cha vipaumbele vya sera. Kazi katika kilimo na maeneo ya vijijini imekuwa kipaumbele cha kwanza katika ajenda kwa miaka 19 mfululizo tangu Mwaka 2004.
Waraka huo unataka kuongezwa kwa juhudi ili kuleta utulivu na kuongeza uzalishaji katika shughuli za kilimo, kuongeza kwa kasi mapato ya wakulima, na kuhakikisha utulivu katika maeneo ya vijijini ya China ili kukabiliana na janga la UVIKO-19 na mabadiliko mengine ambayo hayajapata kutokea katika kipindi cha karne iliyopita na kukuza maendeleo bora ya uchumi na jamii.
"Lazima tushikilie kithabiti misingi ya kudhamini usalama wa nafaka wa China na kuhakikisha hakuna watu wengi kurudi kwenye hali ya umaskini," waraka huo unabainisha.
Waraka unasema, China itaimarisha uzalishaji wa nafaka na usambazaji wa bidhaa muhimu za kilimo.
Waraka huo unasema kwamba, katika Mwaka wa 2022, China inalenga kuendeleza hekta milioni 6.67 za mashamba ya kiwango cha juu, kukuza miradi ya taifa ya ulinzi wa udongo mweusi, na kuzindua sensa ya tatu ya hali ya udongo nchini kote.
Pia waraka huo unataja hatua za kukuza kwa nguvu utafiti wa teknolojia muhimu za kilimo kama vile seli na jini za mimea, kuimarisha matumizi ya mashine na vifaa vya kilimo, kuharakisha maendeleo ya kilimo cha msingi, na kuzuia na kukabiliana ipasavyo na majanga makubwa yanayohusiana na kilimo.
Waraka huo unahimiza juhudi za kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na kuwasaidia watu walio katika hatari ya kurejea katika umaskini, na kuhakikisha sera za msaada na uungaji mkono zinatekelezwa kwa wakati.
Waraka unasema, China itaongeza uungwaji mkono kwa maeneo muhimu katika ustawishaji wa vijijini na kwa jamii za watu waliohamishwa huku ikifanya kazi ya kukuza maendeleo jumuishi ya viwanda vya msingi, vya pili na vya tatu katika maeneo ya vijijini.
Katika mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua, Waziri wa Kilimo na Masuala ya Vijijini Tang Renjian amesema nchi inapaswa kuimarisha mafanikio ya kupunguza umaskini juu ya msingi wa ukuaji wa uchumi, pamoja na msaada zaidi wa kifedha katika kukuza teknolojia, vifaa na masoko ya bidhaa za viwanda za vijijini ambavyo vitasaidia kuongeza mapato ya familia za vijijini.
Tang ameorodhesha usindikaji wa mazao ya shambani, utalii wa vijijini na biashara za mtandaoni za vijijini kama sekta tatu kuu za kuboresha maisha vijijini, na amesisitiza kuzuia matumizi ya fedha kupindukia, maendeleo na ujenzi kupita kiasi, ili kutoa matokeo halisi.
Waraka huo pia umehimiza kuendelea kwa utekelezaji wa mpango kazi wa miaka mitano wa kuboresha mazingira ya makazi vijijini, ukisisitiza kazi muhimu ya kuimarisha miundombinu ya vijijini katika maeneo muhimu kama barabara kuu, miundombinu ya maji, gridi ya umeme na vifaa vya nishati safi, pamoja na kuinua kiwango cha mazingira ya makazi ya vijijini.
Waraka unasisitiza kwamba, kazi zaidi itafanywa ili kuimarisha ujenzi wa mfumo wa mikopo vijijini na kuwezesha ukopeshaji wa mikopo kwa kaya za vijijini, huku bima ya kilimo na bima nyingine zitahimizwa kikamilifu.
Waraka huo pia umependekeza kuboresha mifumo ya uajiri na mafunzo ya watu ili kukuza vipaji vijijini.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma