Kenya yafungua tena njia ya kurukia ndege katika uwanja wa Jomo Kenyatta baada ya kufungwa kwa muda mfupi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 24, 2022

NAIROBI - Mamlaka ya usafiri wa anga nchini Kenya imesema Jumatano jioni kuwa imefungua tena njia ya kurukia ndege ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kufuatia kufungwa kwa muda mfupi baada ya ndege kupata hitilafu ya kimitambo.

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Kenya (KAA) imesema njia ya kurukia ndege imesafishwa ili kuruhusu shughuli za kawaida katika uwanja wa JKIA kurejea.

"Njia ya ndege ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta imesafishwa na kufunguliwa. Shughuli za kawaida zimeanza tena," KAA imesema katika taarifa fupi iliyotolewa Nairobi, Mji Mkuu wa Kenya.

Mamlaka ya usafiri wa anga iliwashauri abiria ambao safari zao za ndege zimeathirika kuwasiliana na mashirika ya ndege ili kujua hali zao za safari.

Kufungwa kwa muda kwa njia ya ndege kulitatiza kutua na kupaa kwa ndege, hivyo kulazimisha mamlaka hiyo ya usafiri wa anga kuzielekeza ndege za abiria kutua kwenye viwanja vingine vya ndege.

Maafisa katika uwanja huo wa ndege walisema ndege zote zinazopaswa kutua zinaelekezwa katika mji wa pwani wa Mombasa huku maafisa wakiendelea na kazi ya kuiondoa ndege ya Fly540 kwenye njia ya kurukia.

Jioni ya Jumatano wiki hii KAA ilifunga kwa muda njia ya kurukia ndege katika uwanja huo baada ya ndege ya Fly540 kupata hitilafu ya kiufundi.

KAA ilisema safari za ndege kwenda na kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) zilikatizwa kwa saa kadhaa baada ya ndege hiyo kukwama kwenye njia ya kurukia ndege.

Mkurugenzi Mkuu wa KAA Gilbert Kibe alisema kuondoka na kuwasili kwa ndege kumeathiriwa, akibainisha kuwa ni ndege ndogo pekee zinazoweza kupaa kupitia njia ya 24.

Aliongeza kuwa mafundi walikuwa wanalifanyia kazi suala hilo ili kutatua hitilafu ya kiufundi iliyojitokeza.

Tukio hilo lilisababisha masikitiko mengi kwa wasafiri, haswa wale wanaounganisha safari kwenda maeneo mengine.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha