Mbio za mwenge wa Michezo ya Olimpiki ya walemavu ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 kuanza Jumatano

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 02, 2022

BEIJING – Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki na Michezo ya Olimpiki ya walemavu ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 Jumanne wiki hii imetoa taarifa kwamba, mbio za Mwenge wa Michezo ya Olimpiki ya walemavu ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 zimepangwa kuanza leo Jumatano Machi 2 hadi 4, na wakimbiza mwenge 565 watashiriki katika maeneo ya mashindano ya Beijing, Yanqing na Zhangjiakou.

Mkimbiza mwenge Aileen Neilson, anayetumia kiti cha magurudumu, akitazama mwenge wakati wa Sherehe za Kuwasha Moto wa asili wa Michezo ya Olimpiki ya walemavu ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022 huko Stoke Mandeville, Uingereza, Februari 28, 2022. Moto wa asili wa Michezo ya Olimpiki ya walemavu ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 uliwashwa Jumatatu wiki hii huko Stoke Mandeville, kijiji kilichoko Kaskazini Magharibi mwa London ambacho kinatambuliwa kuwa mahali pa kuzaliwa kwa Michezo hiyo. (Xinhua/Li Ying)

Wakati Moto wa asili wa Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 ukiwashwa Jumatatu wiki hii huko Stoke Mandeville, kijiji kilichoko Kaskazini Magharibi mwa London ambacho kinatambuliwa kuwa mahali pa kuzaliwa kwa Michezo ya Olimpiki ya walemavu, moto huo pia utakusanywa na mioto mingine katika maeneo mengine manane huko Beijing na Zhangjiakou. Kila mkusanyo utafuatwa na mbio za mwenge kwa wakimbiza mwenge wasiozidi 20 katika eneo husika kabla ya kukusanyika kwa mioto yote tisa kwenye Bustani ya Tiantan.

Asubuhi ya Alhamisi wiki hii, mbio za mwenge zitafanyika katika maeneo manne mjini Zhangjiakou, na mchana mbio za mwenge zitafanyika katika maeneo mawili mjini Beijing, ikiwa ni pamoja na eneo la Kusini la Hifadhi ya Misitu ya Olimpiki lililoko ndani ya maeneo ya kitanzi ya michezo hiyo, ambapo zaidi ya wakimbiza mwenge 20 kutoka Familia ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki ya Walemavu (IPC) watapokezana mwenge huo.

Siku ya Ijumaa, mbio za mwenge zitaendelea katika maeneo mengine matatu yakiwemo Makao Makuu ya Kamati ya Maandalizi ya michezo hiyo ya Beijing 2022 (BOCOG).

Kwa mujibu wa Yan Cheng, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa BOCOG, wakimbiza mwenge 565 walisajiliwa na kuchaguliwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), BOCOG, Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu la China, Mji wa Beijing na Mkoa wa Hebei, huku asilimia 21 ya wakimbiza mwenge hao wakiwa ni watu wenye ulemavu, idadi ambayo ni zaidi ya mahitaji ya IPC ya asilimia 15.

Wakati wa mbio za mwenge, baadhi ya watu wenye ulemavu watatumia roboti za kuwasaidia kubeba mwenge. Baada ya miezi kadhaa ya mafunzo ya kukabiliana na hali kwa kutumia vifaa hivyo, wanaweza kushika mwenge mwenyewe na kutembea wima.

Naibu Katibu Mkuu wa BOCOG Xu Zhijun amesema njia hiyo inawasilisha dhana ya "teknolojia hubadilisha maisha na kufanya visivyowezekana viwezekane" kwa watu wenye ulemavu, ambayo pia inaendana na dhana ya mbio za mwenge wa Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Majira ya baridi ya Beijing.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha