Tanzania yauza nje zaidi ya tani 5,000 za nyama katika kipindi cha miezi saba

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 08, 2022

DAR ES SALAAM - Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania, Mashimba Ndaki amesema Jumatatu wiki hii kwamba, nchi hiyo iliuza nje tani 5,362.9 za nyama zenye thamani ya dola za Marekani 22,442,111.96 kati ya Julai 2021 na Januari 2022.

"Ongezeko la asilimia 200 la mauzo ya nyama ni habari njema kwa nchi na wazalishaji wa nyama ambao wanatazamia mustakabali mwema," Ndaki amewaambia waandishi wa habari kwenye mkutano wa wanahabari uliofanyika Dodoma, Mji Mkuu wa Tanzania.

Amehusisha ongezeko hilo la mauzo ya nyama nje ya nchi na kuboreshwa kwa sera na mikakati katika biashara ya nyama iliyowekwa na utawala wa nchi hiyo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Ndaki amesema, nyama hiyo ilisafirishwa kwenda kuuzwa katika nchi za Comoro, Saudi Arabia, Vietnam, Qatar, China, Bahrain, Kuwait na Oman.

Kuhusu uzalishaji wa maziwa, Ndaki amesema viwanda vya kusindika maziwa vimeongezeka na kufikia 105 kutoka 99 katika kipindi hicho na hivyo kuzalisha lita 207,951 kwa siku.

Amesema uzalishaji wa bidhaa za ngozi pia umeimarika kwa kiasi kikubwa kufuatia ujenzi wa viwanda zaidi ya viwili vya kisasa vya kusindika ngozi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Tanzania kwa sasa ina ng’ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.29 na kondoo milioni 5.65. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha