China yahimiza ushirikiano na mazungumzo huku hali ya kutokuwa na uhakika ikiongezeka duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 08, 2022

Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi akihudhuria mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya video kuhusu sera ya mambo ya nje na uhusiano wa nje wa China pembezoni mwa mkutano wa tano wa Bunge la Umma la 13 la China (NPC) kwenye Jumba la Mikutano la Umma la Beijing, Mji Mkuu wa China, Machi 7, 2022. (Xinhua/Chen Zhonghao)

BEIJING - Kutokana na mabadiliko makubwa ambayo hayajapata kuonekana katika kipindi cha karne moja, China siku ya Jumatatu wiki hii imetoa wito kwa nchi duniani kuendelea kujitolea kusitisha vita kwa njia ya mazungumzo, kusuluhisha migogoro kwa njia ya mazungumzo, na kuongeza hali ya kuaminiana kupitia ushirikiano.

Ujumbe huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi katika mkutano na waandishi wa habari pembezoni mwa "mikutano mikuu miwili" ya kila mwaka inayoendelea nchini humo.

Uhusiano na nchi kubwa

Akijibu swali kuhusu uhusiano wa China na Russia, Wang amesema nchi hizo mbili zitadumisha mwelekeo wa kimkakati na kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kiwenzi na wa kimkakati kwa pande zote kati ya China na Russia katika zama mpya.

Amebainisha kuwa uhusiano kati ya China na Russia umejikita katika mantiki ya wazi ya historia na unasukumwa na mienendo ya ndani ya nchi hizo, na urafiki kati ya watu wa China na Russia ni imara.

Juu ya uhusiano kati ya China na Marekani, Wang amesema nchi hizo mbili zinapaswa kubadili uhusiano wa sasa wa "ushindani-ushirikiano-uadui" kuwa uhusiano wa kanuni tatu za kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na ushirikiano wa kunufaishana.

Wang akiilaumu Marekani kuunda vikundi dhidi ya China, amekosoa vikali mkakati wa Marekani kuhusu eneo la Bahari ya Hindi na Pasifiki akiufananisha na aina mpya ya NATO barani Asia na kwamba unadhoofisha muundo wa ushirikiano wa kikanda unaozingatia ASEAN, na kuathiri maslahi ya jumla na ya muda mrefu ya nchi katika kanda hiyo.

Wang amepongeza uhusiano wenye matokeo mengi kati ya China na Ulaya, akisema mazungumzo na ushirikiano kati ya pande hizo mbili juu ya msingi wa kuheshimiana na kunufaishana yataleta utulivu zaidi kwa dunia yenye msukosuko. Pia amesema, ushirikiano kati ya China na Ulaya unatokana na uungaji mkono thabiti wa umma, maslahi mapana ya pamoja, na mahitaji sawa ya kimkakati.

Ushirikiano katika mwaka wenye changamoto

Wang amesifu uhusiano kati ya China na nchi za ASEAN, Afrika na Latin Amerika.

Wang amesema, China na Jumuiya ya Nchi za Asia ya Kusini Mashariki (ASEAN) zimeanzisha mfano wa ushirikiano wa kikanda wenye nguvu na wenye mustakabali mzuri zaidi katika miongo mitatu iliyopita.

Kuhusu ushirikiano kati ya China na Afrika, Wang amesema China inaheshimu ahadi yake ya kushirikiana na nchi za Afrika na kamwe haitoi ahadi tupu.

Wang amesema, kwa miaka mingi, China imejenga zaidi ya kilomita 10,000 za reli, hadi kilomita 100,000 za barabara kuu, karibu bandari 100, na hospitali na shule zisizohesabika barani Afrika, "Hizi siyo 'mitego ya madeni,' bali ni minara ya ushirikiano."

Wang pia amepongeza ushirikiano kati ya China na Amerika ya Kusini na eneo la Caribbean (LAC), akisema kuwa LAC ni eneo lenye matumaini na uhai na siyo miliki ya mtu yeyote.

"Wanachohitaji watu katika eneo hili ni haki na ushirikiano wa kunufaishana, siyo siasa za madaraka, uasi au uonevu," Wang amesema.

Picha iliyopigwa Septemba 11, 2021 inaonyesha Banda la Kimataifa la "Ukanda Mmoja na Njia Moja" katika Maonesho ya 18 ya China-ASEAN huko Nanning, Guangxi nchini China. (Xinhua/Lu Boan)

Ukraine na Masuala mengine

Wang Yi huku akisema China inachukua jukumu la kiujenzi, ametoa mapendekezo sita kuhusu Ukraine, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha shughuli za kibinadamu zinazingatia kanuni ya kutoegemea na kupendelea upande wowote, kuzingatia mahitaji ya kibinadamu ya watu wanaokimbia vita kutoka Ukraine, na kuunga mkono uratibu wa Umoja wa Mataifa (UN) katika jukumu la kuelekeza misaada ya kibinadamu na kazi ya mratibu wa UN wa mgogoro wa Ukraine.

Kuhusu suala la Afghanistan, Wang amesema, vipaumbele vya haraka ni kutoa msaada wa kibinadamu huku akiitaka Marekani kuondoa mara moja kizuizi cha mali za Afghanistan nchini Marekani na vikwazo mbalimbali vya upande mmoja.

Kuhusu Peninsula ya Korea, Wang amesema, vitisho vya usalama vya nje vinavyoikabili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK) vimesalia bila kushughulikiwa na masuala yake halali ya kiusalama hayajatatuliwa kwa muda mrefu.

"Tumeona kuwa upande wa Marekani hivi karibuni umesema kuwa hauna nia ya chuki dhidi ya DPRK na uko tayari kutatua suala hilo kupitia njia za kidiplomasia, ambazo zinastahili kupongezwa," Wang amesema. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha