

Lugha Nyingine
Tanzania yarekodi ukuaji wa kasi katika sekta ya madini Mwaka 2021
DAR ES SALAAM - Doto Biteko, Waziri wa Madini wa Tanzania amesema kwamba, mchango wa sekta ya madini ya nchi hiyo katika uchumi wa taifa uliongezeka hadi kufikia asilimia 7.3 Mwaka 2021 kutoka asilimia 6.5 ya Mwaka 2020.
Biteko amesema kwamba, matarajio ya serikali ni kuona sekta ya madini inachangia asilimia 10 katika uchumi wa taifa ifikapo Mwaka 2025 lakini hilo linaweza kufikiwa mapema zaidi.
Biteko amewaambia waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika Alhamisi wiki hii katika Mji Mkuu wa Dodoma kuwa sekta ya madini iliweka historia katika mwaka mmoja uliopita ambapo mauzo ya madini yalifikia shilingi za Tanzania trilioni 8.3 (kama dola za Marekani bilioni 3.6) na serikali kukusanya kodi na mrabaha wa shilingi za Tanzania bilioni 597.53.
Biteko amesema ushiriki wa Watanzania katika huduma za sekta ya madini uliongezeka kutoka asilimia 43 hadi asilimia 63 wakati mapato ya huduma za madini yalikuwa dola za Marekani milioni 579.3.
Amesema mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya madini yametokana na mageuzi yaliyofanywa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni pamoja na kuboreshwa kwa hali ya uchimbaji madini kwa wachimbaji wadogo ambao walichangia asilimia 30 ya shughuli za uchimbaji madini nchini humo.
Biteko amesema mageuzi hayo yamewezesha kujengwa kwa vituo visivyopungua 44 vya biashara ya dhahabu na vituo vingine 70 vya biashara ya madini nchi nzima ambavyo vimesaidia kukomesha utoroshaji wa madini nje ya nchi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma