Serikali ya Hong Kong yaongeza msaada kwa watu walio chini ya karantini ya nyumbani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 14, 2022

HONG KONG – Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mkoa wa Utawala Maalumu wa Hong Kong (HKSAR) nchini China Carrie Lam amesema kuwa, Hong Kong itaendelea kuimarisha msaada kwa watu walio chini ya karantini kutokana na UVIKO-19.

Lam amesema Jana Jumapili wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu hatua za kupambana na janga la virusi vya Korona kwamba takriban watu 300,000 kwa sasa wako kwenye karantini ya nyumbani, ingawa takwimu hii inaweza kuwa si halisi kwani baadhi yao wameshakamilisha kujitenga kijamii.

"Serikali ya HKSAR imeendelea kuimarisha uwezo wake wa kusaidia watu hawa wa nyumbani, lakini bado 'tunajitahidi'," amesema Lam.

Kwa mujibu wa Lam, kwa sasa msaada kwa watu walio chini ya karantini ya nyumbani unahusu usambazaji wa vifaa vya kujikinga dhidi ya janga na huduma ya namba ya simu ya mawasiliano ya dharura, ambapo usambazaji wa vifaa kwenda majumbani hufanyika pale inapolazimu baada ya tathmini ya Serikali ya HKSAR.

Lam amesema, Serikali ya Hong Kong pia itatoa msaada wa kimatibabu ikiwa ni pamoja na msaada wa kisaikolojia, tathmini ya afya, mashauriano ya mbali, pamoja na kukubali miadi katika kliniki zilizoteuliwa za Mamlaka ya Hospitali.

Alfred Sit, Waziri wa Uvumbuzi na Teknolojia wa Serikali ya HKSAR, amesema kuwa Serikali ya HKSAR tayari imesambaza vifaa vya kujikinga dhidi ya janga, ambavyo ni pamoja na barakoa, vipimo vya haraka vya antijeni, vipima joto na dawa za mitishamba za Kichina, na vinginevyo, kwa wagonjwa zaidi ya 460,000 na wale waliokutana kwa ukaribu na wagonjwa hao tangu Februari 21.

"Serikali ya HKSAR itaharakisha usambazaji wa vifaa vya kukabiliana na janga huku kukiwa na ongezeko la wagonjwa walioambukizwa tangu mwishoni mwa Februari," Sit amesema.

Idara ya Mambo ya Ndani ya Serikali ya HKSAR imeanzisha nambari ya mawasiliano ya simu kwa saa 24 mnamo Februari, ikitoa msaada kwa watu walio katika karantini ya nyumbani chini ya kampeni ya "Baki Nyumbani Salama".

“Idadi ya simu za dharura imeongezwa kutoka 100 hadi 280, huku watu 540 wakishughulikia masuala kutoka kwa watu zaidi ya 10,000 kila siku” amesema Jack Chan, Kaimu Waziri wa masuala ya Mambo ya Ndani wa Serikali ya HKSAR, akiongeza kuwa wanapanga kuongeza idadi ya simu hadi 550 wakati ujao.

Mamlaka ya Hospitali ya Hong Kong pia imefungua laini 110 za mawasiliano ya msaada wa dharura na kushughulikia zaidi ya masuala 25,000 kufikia Machi 11, na mipango ya kuongeza idadi ya laini za simu za msaada hadi 200 ili kujibu mahitaji ya umma.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha