

Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa China asisitiza umuhimu wa ukuaji thabiti wa uchumi
BEIJING - Waziri Mkuu wa China Li Keqiang jana Jumatatu wakati akiongoza mkutano wa utendaji wa Baraza la Serikali la China amesisitiza umuhimu wa juhudi za kukabiliana na changamoto ili kuhakikisha ukuaji thabiti wa uchumi.
Mkutano huo umesambaza vipaumbele vilivyowekwa katika ripoti ya kazi ya serikali ya mwaka huu kwa vyombo husika vya Baraza la Serikali la China na serikali za mitaa, na kutaka utekelezaji thabiti.
Kwa kutambua kwamba uchumi unakabiliwa na shinikizo jipya la kushuka na changamoto zinazoongezeka, mkutano huo umesisitiza haja ya kuratibu juhudi za kuzuia na kudhibiti janga la UVIKO-19 na maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na hitaji la kuweka katika kipaumbele cha juu zaidi jukumu la kuhakikisha ukuaji thabiti wa uchumi.
Ili kufikia lengo hili, China itafuatilia kwa karibu mabadiliko ya hali ya uchumi duniani, marekebisho ya sera kuu za uchumi wa jumla, mwelekeo wa soko wa bidhaa kubwa, na athari za mambo haya kwa China.
Mkutano umeeleza kuwa, China itaendelea kuboresha hatua zake za kukabiliana na hali mbalimbali ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi na ajira, na kuweka bei za bidhaa ndani ya kiwango kinachofaa.
Mkutano huo umetoa wito wa kutekelezwa kwa kina kwa sera za jumla ili kuweka shughuli za wadau wa soko katika uthabiti na kukuza utulivu wa ajira.
Mkutano pia umesisitiza kwamba, urejeshaji wa malipo ya kodi na upunguzaji wa kodi ni hatua muhimu kwa mwaka huu ili kudumisha utendaji thabiti wa uchumi wa jumla. Imeelezwa kwamba, mpango wa kina wa urejeshaji wa kodi ya ongezeko la thamani utaandaliwa na kuzinduliwa haraka iwezekanavyo.
Kwa mujibu wa mkutano huo, taasisi za kifedha zinapaswa kuongozwa ili kutekeleza hatua zinazolenga biashara za kati na ndogo, kwa nia ya kufanya upatikanaji wa fedha kuwa rahisi na kupunguza gharama za kukusanya mitaji.
Juhudi zitafanywa ili kuongeza mahitaji ya ndani, kufungua uwezekano wa manunuzi na matumizi ya bidhaa na kuongeza uwekezaji mzuri.
Mkutano umesema, ugavi thabiti wa makaa ya mawe na umeme utahakikishwa.
Umesisitiza juhudi za kuimarisha usimamizi wa soko, kulinda ushindani wa haki, na kufikia mafanikio katika teknolojia muhimu.
Mkutano huo pia umesisitiza haja ya kujumuisha na kupanua mafanikio katika kupunguza umaskini, na kutekeleza hatua zinazohusu elimu ya lazima, matibabu ya kimsingi, makazi ya msingi na maeneo mengine ili kuhakikisha mahitaji ya kimsingi ya watu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma