Benki ya Dunia yatoa dola milioni 750 Kwa Kenya ili kuchochea ongezeko la uchumi baada ya janga

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 18, 2022

NAIROBI - Benki ya Dunia imeidhinisha shilingi bilioni 85.77 (kama dola milioni 750 za Kimarekani) kwa Kenya ili kusaidia kuharakisha ufufukaji wa uchumi unaoendelea na ulio imara kutokakana na athari za janga la UVIKO-19.

Benki ya Dunia imesema katika taarifa iliyotolewa Alhamisi wiki hii kwamba Operesheni ya Sera ya Maendeleo (DPO) itasaidia Kenya kuimarisha uendelevu wa kifedha kupitia mageuzi ambayo yanachangia uwepo wa uwazi zaidi na vita dhidi ya ufisadi.

Keith Hansen, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Kenya, Rwanda, Somalia na Uganda, amesema kuwa serikali imedumisha kasi ya kufanya mageuzi muhimu licha ya changamoto zinazosababishwa na janga hilo.

"Benki ya Dunia, kupitia chombo cha DPO, inafuraha kuunga mkono juhudi hizi ambazo zinaiweka Kenya katika nafasi nzuri ya kuendeleza ufanisi wake wa ukuaji wa uchumi na kuielekeza kwenye maendeleo jumuishi na ya kijani," amesema Hansen.

DPO ni ya pili katika sehemu mbili za shughuli za maendeleo zilizoanzishwa Mwaka 2020 ambazo hutoa ufadhili wa bajeti ya gharama nafuu pamoja na usaidizi wa marekebisho muhimu ya sera na taasisi.

Inalenga mageuzi ya sekta mbalimbali katika mihimili mitatu -- mageuzi ya fedha na madeni ili kufanya matumizi kuwa ya uwazi na yenye ufanisi zaidi na kuimarisha ufanisi wa soko la madeni la ndani; mageuzi ya sekta ya umeme na ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kuiweka Kenya kwenye njia bora ya kutumia nishati safi, na kuimarisha uwekezaji wa miundombinu ya kibinafsi; na kuimarisha mfumo wa usimamizi wa rasilimali asili na rasilimali ya watu wa Kenya ikijumuisha mazingira, ardhi, maji na huduma za afya.

Benki hiyo imesema DPO pia inaunga mkono uwezo wa Kenya wa kushughulikia magonjwa ya milipuko ya siku zijazo kupitia kuanzishwa kwa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Umma ya Kenya (NPHI), ambayo itaratibu shughuli na programu za afya ya umma ili kuzuia, kugundua, na kukabiliana na matishio ya afya ya umma, ikiwemo magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, na matukio mengine ya afya.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha