

Lugha Nyingine
Bado hakuna manusura waliopatikana katika ajali ya ndege iliyotokea China huku uokoaji ukiendelea
Picha iliyopigwa kwa simu ikionyesha mkutano na waandishi wa habari kuhusu ajali ya ndege aina ya Boeing 737 ya shirika la ndege la China Eastern Airlines huko Wuzhou, Mkoa wa Guangxi nchini China, Machi 22, 2022. Afisa wa Idara ya Usafiri wa Anga ya China amesema Jumanne jioni kwamba, hadi kufikia sasa hakuna manusura waliopatikana baada ya ndege ya abiria iliyokuwa na watu 132 kuanguka Kusini mwa China katika Mkoa wa Guangxi. (Xinhua/Liang Shun)
NANNING – Afisa wa Idara ya Usafiri wa Anga ya China amesema kwamba, hadi sasa hakuna manusura waliopatikana baada ya ndege ya abiria iliyokuwa na watu 132 kuanguka mkoani Guangxi Kusini mwa China.
Zhu Tao, Mkuu wa ofisi ya usalama wa anga ya Idara ya Usafiri wa Anga ya China (CAAC), amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba, ndege aina ya Boeing 737 ya Shirika la Ndege la China Eastern Airlines iliyokuwa ikitoka Kunming kuelekea Guangzhou, ilidumisha mwinuko wa mita 8,900 ilipoingia katika eneo la udhibiti wa usafiri wa anga la Guangzhou saa 8 na dakika 17 mchana wa Jumatatu wiki hii, lakini iligundulika kuwa ilianguka saa 8 na dakika 20.
Kwa mujibu wa Zhu, wadhibiti wa safari za anga walipiga simu mara kwa mara kwa wafanyakazi wa ndege hiyo, lakini hazikupokelewa. Ndege hiyo ilipoteza mawimbi kwenye rada saa 8 na dakika 23 mchana, na baadaye iligundulika kuwa ilianguka katika Kaunti ya Tengxian katika Mji wa Wuzhou.
“Hakuna raia wa kigeni waliokuwa kwenye ndege hiyo yenye namba ya usajili MU5735” amesema Zhu, na kuongeza kuwa watu 132 waliokuwa ndani walikuwa abiria 123 na wafanyakazi tisa.
“Kwa mujibu wa taarifa zinazojulikana, idara bado haina ufahamu wa kutosha kuhusu chanzo cha ajali hiyo,” amesema Zhu. "Uchunguzi ni mgumu sana kwani ndege hiyo iliharibiwa vibaya."
Zhu amesema, kwa sasa, timu ya uchunguzi inafanya uchunguzi kamili kwa utaratibu, huku waokoaji wakichunguza eneo zima la ajali na kwenda sehemu zote kutafuta masanduku meusi yenye taarifa muhimu kuhusu ndege hiyo.
“Timu hiyo pia inachunguza kwa kina masuala mengine ya ajali, ikiwa ni pamoja na ndege yenyewe, ukarabati, udhibiti wa safari za anga, hali ya hewa, ubunifu na utengenezaji wa ndege” Zhu amesema.
Sun Shiying, Mwenyekiti Shirika la ndege la China Eastern Airlines tawi la Mkoa wa Yunnan amesema katika mkutano huo kuwa mawasiliano na familia za abiria wote 123 yalifanywa ndani ya masaa 24 baada ya ajali.
Zaidi ya watu 2,000 wamejiunga na shughuli ya uokoaji katika eneo hilo.
Siku ya Jumanne, Kampuni ya Boeing ya China, ilisema kuwa inashirikiana na Shirika la ndege la China Eastern Airlines, na wataalam wake wa kiufundi wako tayari kusaidia CAAC katika kufanya uchunguzi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma