

Lugha Nyingine
Xi aongoza mkutano wa viongozi wa CPC kuhusu hatua za dharura za ajali ya ndege ya hivi majuzi nchini China
BEIJING - Kamati ya Kudumu ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Alhamisi wiki hii imefanya mkutano ili kusikiliza ripoti kuhusu hatua za dharura zilizochukuliwa kwenye ajali ya hivi majuzi ya ndege ya Shirika la China Eastern Airlines.
Xi Jinping, Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya CPC, ameongoza mkutano huo, ambao uliunda kikosi kazi cha kufuatilia utekelezaji.
Baada ya kutokea kwa ajali hiyo ya ndege, Xi aliamuru kutekelezwa mara moja kwa hatua za kukabiliana na hali ya dharura, juhudi za kutafuta na kuokoa, na suluhu ifaayo baada ya ajali hiyo, akihimiza juhudi za kuchunguza chanzo cha ajali hiyo, kuzifariji familia za waathirika na kuwapa msaada.
Mkutano huo umesema, idara husika zimetekeleza agizo hilo haraka ili kuhamasisha nguvu katika maeneo ya usafiri wa ndege na hatua za dharura kufanya kazi zinazohusika .
Hivi sasa, utatuzi wa matokeo na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea kwa utaratibu.
Mkutano umetoa wito wa kuweka watu na maisha yao mbele katika kushughulikia athari za tukio hilo, ambalo lilisababisha vifo vya watu 132.
“Kazi inayofuata, ikiwa ni pamoja na kutambua na kurejesha mabaki ya waathirika, inapaswa kufanywa vizuri” mkutano huo umesema.
Mkutano umesisitiza kwamba, uchunguzi lazima ufanyike kwa njia ya kisayansi na kwa utaratibu unaofaa, huku wataalam wakielekezwa kujiandaa kwa kina kuchambua data za ndege na ushahidi mbalimbali ili kujua sababu na chanzo cha ajali hiyo haraka iwezekanavyo.
“Wakati huo huo, taarifa zinazohusiana zinapaswa kutolewa kwa wakati, kwa usahihi, na uwazi ili kujibu maswali kutoka kwa umma” mkutano umesema.
Mkutano huo uumesisitiza kuwa maendeleo hayapaswi kamwe kuja kwa gharama ya usalama, na kuwataka wahusika wanaohusika kujifunza kutoka kwenye tukio hilo na kufanya ukaguzi juu ya usalama wa uzalishaji nchi nzima.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma