OPEC+ yasema itaendelea kuzalisha mafuta kwa kiwango cha wastani licha ya kupanda kwa bei

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 01, 2022

VIENNA - Shirika la Nchi Zinazouza Petroli (OPEC) na washirika wake, kundi linalojulikana kama OPEC+, limetangaza kwamba litazingatia mipango iliyopo ya ongezeko la wastani la uzalishaji wa mafuta katika kipindi cha Mwezi Mei licha ya kupanda kwa bei mafuta ghafi.

OPEC+ imethibitisha tena "uamuzi wa kurekebisha ongezeko la uzalishaji wa kila mwezi kwa mapipa 432,000 kwa siku kwa Mwezi wa Mei 2022," kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya Mkutano wa 27 wa Mawaziri wa OPEC na wasio wa OPEC.

Hadi kufikia sasa, OPEC+ imeongeza mapipa 400,000 kwa siku mwanzoni mwa kila mwezi, kwa mujibu wa ratiba yake ya ongezeko la taratibu lililokubaliwa Mwezi Julai, 2021 ili kufidia upunguzaji wa uzalishaji uliofanywa wakati wa kilele cha janga la UVIKO-19 Mwaka 2020.

Taarifa ya OPEC+ imesema, ongezeko kidogo la uzalishaji kwa Mwezi Mei linatokana na viwango vya uzalishaji vilivyorekebishwa, ambavyo pia vilikubaliwa na nchi wanachama Mwezi Julai mwaka jana.

Muungano huo pia umeeleza katika taarifa yake kwamba kuyumba kwa sasa katika soko la mafuta kunasababishwa na maendeleo ya siasa za kijiografia badala ya mabadiliko katika misingi ya soko.

"Kuendelea kwa misingi ya soko la mafuta na makubaliano juu ya mtazamo kumelifanya soko kuwa lenye uwiano mzuri," imesema taarifa hiyo.

Katika wiki za hivi karibuni, bei ya mafuta imepanda kwa kiasi kikubwa ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa miaka mingi kutokana na mahitaji ya ufufukaji wa uchumi wa Dunia na hofu kuhusu kuvurugika kwa usambazaji inayotokana na mgogoro wa Russia na Ukraine.

Mataifa yanayotumia mafuta kwa kiasi kikubwa yakiwemo Marekani, Uingereza na Ujerumani hivi majuzi yametoa wito kwa nchi za OPEC+ kuongeza malengo yao ya uzalishaji ili kudhibiti kupanda kwa bei. Hata hivyo, nchi wanachama wakuu ikiwemo Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimekataa wito huo na kusisitiza kuzingatia utaratibu wa OPEC+.

Katibu Mkuu wa OPEC Mohammad Barkindo Jumatano wiki hii alihimiza OPEC+ "kubakia katika mkondo" wa maamuzi ya muungano huo, kuwa makini katika kufuatilia mabadiliko ya hali ya soko na kuweka mkazo katika kusawazisha soko.

Barkindo pia alitoa wito kwa viongozi wa kimataifa kuzingatia mfumo wa uhusiano wa pande nyingi ili kuhakikisha mtiririko wa nishati "usio na vizuizi, dhabiti na salama" kwenye soko la kimataifa. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha