Mfumuko wa bei wa China waendelea kuwa tulivu licha ya shinikizo la kiuchumi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 12, 2022

Wakazi wakinunua mboga katika duka kubwa lililoko Eneo la Putuo, Shanghai, China, Machi 31, 2022. (Xinhua/Liu Ying)

BEIJING – Takwimu rasmi za Serikali ya China zilizotolewa Jumatatu wiki hii zinaonesha kuwa, mfumuko wa bei wa China kwa ujumla umedumisha utulivu mwezi Machi licha ya kuibuka tena na mara kwa mara kwa maambukizi ya virusi vya Korona na kupanda kwa bei za bidhaa nyingi katika soko la kimataifa.

Idara ya Taifa ya Takwimu ya China (NBS) imesema kuwa, kielezo cha bei kwa wanunuzi nchini China (CPI), ambacho ndicho kipimo kikuu cha mfumuko wa bei, kilipanda kwa asilimia 1.5 mwezi Machi ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Kiwango hicho ni kikubwa kuliko ukuaji wa asilimia 0.9 wa mwaka hadi mwaka uliorekodiwa mwezi Februari.

“Mchanganuo wa data unaonyesha kuwa bei za vyakula zilipungua hadi asilimia 1.5 mwaka hadi mwaka, na hivyo kushusha CPI chini kwa asilimia 0.28” amesema Dong Lijuan, mtakwimu mwandamizi wa NBS.

Data zinaonesha kuwa, hasa, bei ya nyama ya nguruwe, nyama inayoliwa zaidi nchini China, ilishuka kwa asilimia 41.4 mwaka hadi mwaka, ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 42.5 mwezi uliopita. Hata hivyo, bei za mboga, ambayo ilishuka kwa asilimia 0.1 Februari, iliongezeka kwa asilimia 17.2 mwezi uliopita.

“Bei zisizo za vyakula zilipanda kwa asilimia 2.2 kutoka mwaka uliopita, na kuchangia takriban asilimia 1.77 ya ukuaji wa CPI” amesema Dong.

"Tokea robo ya kwanza, Serikali ya China imeendelea na jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji ya kila siku ya watu na kuweka utulivu wa bei za mahitaji haya," amesema Wang Likun, mtafiti wa Kituo cha Utafiti wa Maendeleo cha Baraza la Serikali ya China, akibainisha kuwa usambazaji na mahitaji kwa ujumla umeendelea kuwa thabiti.

Tofauti na ongezeko la bei linaloonekana katika uchumi wa nchi nyingine duniani, China imeshuhudia mfumuko wake wa bei ukibaki ndani ya kiwango kinachofaa, anasema Guo Liyan, mtafiti katika Chuo cha Utafiti wa Uchumi mkuu cha China.

"Inaonyesha uthabiti mkubwa wa uchumi wa China, na kiwango chake kikubwa cha soko na hatua madhubuti za nchi kuhakikisha usambazaji bidhaa wa kutosha na bei thabiti," Guo amesema.

Wachambuzi wa uchumi wanaamini kuwa, kwa kuwa na sera za kutosha za kifedha ili kukuza maendeleo ya uchumi na kuongeza imani kwa soko, China inaweza kuzuia hatari zinazoweza kutokea wakati hali ya uchumi inapobadilika.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha