China yarahisisha usimamizi katika kudhibiti UVIKO-19 ili kukidhi mahitaji ya kila siku na ya viwandani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 13, 2022

Mfanyakazi kwa pamoja na mwenzake akiratibu kuwezesha kuondoka kwa treni ya mizigo katika kituo cha mizigo huko Lhasa, Mkoa wa Tibeti nchini China, Aprili 10, 2022. (Xinhua/Zhang Rufeng)

BEIJING - China imechukua hatua kadhaa kuwezesha usimamizi madhubuti ili kuhakikisha usambazaji wa mahitaji muhimu kwa kaya na viwanda wakati wa milipuko ya maambukizi ya virusi vya Korona katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, ambayo yanachukua hatua kali za udhibiti.

Waraka wa Wizara ya Uchukuzi uliotolewa Jumanne wiki hii umepiga marufuku kuzuiwa kwa usafiri wa barabarani au kurudisha nyuma magari au wafanyakazi, bila kujali hali yao, na kuamuru upimaji bora zaidi wa maambukizi ya virusi vya Korona kwenye njia za usafirishaji.

Hatua hizi zimechukuliwa ikiwa ni utekelezaji wa waraka wa Baraza la Serikali ya China uliotolewa mapema Siku ya Jumatatu wiki hii ukihimiza kufanywa kwa juhudi zote zinazowezekana kuhakikisha usafirishaji mzuri wa vifaa vya matibabu na vya kudhibiti janga, mahitaji ya muhimu ya kila siku, usafirishaji kwa haraka wa posta na wa makampuni ya upelekaji, pamoja na rasilimali za uzalishaji, ili kupunguza athari katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Athari katika mnyororo wa ugavi zimejitokeza katika baadhi ya maeneo kutokana na masharti magumu ya usafiririshaji na upimaji wa virusi vya Korona katika kudhibiti janga, huduma za barabara kuu zimesimamishwa, na msongamano wa magari karibu na vibanda vya kupima virusi hivyo kando ya barabara.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, waraka wa Baraza la Serikali ya China uliagiza kutolewa bure kwa huduma za upimaji wa virusi vya Korona kwa madereva wa malori na wafanyakazi wa meli, na vibali vya trafiki vinavyotambuliwa kote nchini kutolewa kwa magari yanayobeba vifaa muhimu.

Serikali za Mitaa zinaendelea kuchukua hatua. Shanghai tayari imeongeza vituo vya kupima virusi vya Korona kando ya barabara kuu na kuweka upendeleo maalumu kwa baadhi ya madereva wa malori mjini humo, huku Bandari ya Shanghai imetoa kibali cha malori ya kubeba kontena kinachokubaliwa na mikoa minne ya karibu katika Delta ya Mto Changjiang.

Majira ya mchipuko wa kilimo ni wakati muhimu wa uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa mwaka mzima, unategemea usambazaji mzuri wa vifaa. Hatua madhubuti zinahitajika ili kuhakikisha wakulima na vifaa vya kilimo vinafika kwa wakati.

Siku ya Jumanne wiki hii, idara nyingine za Serikali ya China pia zilitangaza hatua za kuboresha usimamizi. Shirika la Posta limesisitiza uwasilishaji kwa wakati wa vifurushi vya posta na vya haraka kwa jamii za makazi, na Kamati ya Taifa ya Maendeleo na Mageuzi imesema itahakikisha mahitaji muhimu yanawafikia watu milangoni mwa nyumba zao katika maeneo yaliyoathiriwa na mlipuko wa virusi vya Korona. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha