

Lugha Nyingine
Mapato ya Serikali ya China yaongezeka kwa asilimia 8.6 katika Robo ya Kwanza ya 2022
BEIJING - Takwimu rasmi kutoka Wizara ya Fedha ya China zilizotolewa Jumatano wiki hii zinaonesha kuwa, mapato yatokanayo na kodi na ushuru mbalimbali wa Serikali ya China yaliongezeka kwa asilimia 8.6 katika robo ya kwanza ya Mwaka 2022 kuzidi kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, mapato ya kodi na ushuru ya China yalifikia yuan trilioni 6.2 (kama dola za Kimarekani bilioni 968.81) katika kipindi hicho.
Mapato ya kodi yalifikia yuan trilioni 5.25 katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.7 kulinganishwa na mwaka jana.
Mapato yatokanayo na kodi ya thamani ya nyongeza, ambacho ni chanzo kikubwa zaidi cha mapato nchini humo, yaliongezeka kwa asilimia 3.6 kutoka mwaka uliopita hadi kufikia yuan trilioni 1.92, huku yale ya kodi ya mapato ya mtu binafsi yalifikia yuan bilioni 464.5 katika miezi mitatu ya kwanza, ikiwa ni ongezeko la 16.5 asilimia.
Mapato ya ushuru wa stempu yaliongezeka kwa asilimia 20.6 na kufikia yuan bilioni 156.9 kwa kulinganishwa na mwaka uliopita. Hasa, mapato ya ushuru wa stempu kwenye biashara ya hisa yalirekodi ongezeko la mwaka la asilimia 21.3.
Serikali Kuu na serikali za mitaa zilikusanya yuan trilioni 2.89 na yuan trilioni 3.31 katika mapato ya ushuru na kodi, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.6 na asilimia 9.5, mtawalia.
Takwimu hizo za Jumatano pia zinaonyesha kuwa matumizi ya fedha ya Serikali ya China yalipanda kwa asilimia 8.3 hadi kufikia yuan trilioni 6.36 katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu.
Wizara ya Fedha imesema kuwa, matumizi ya fedha katika elimu yalipanda kwa asilimia 8.5 ikilinganishwa na mwaka uliopita kipindi kama hicho, huku yale ya sayansi na teknolojia yakiongezeka kwa asilimia 22.4.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma