

Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping apongeza mkutano wa kwanza wa China wa kusoma vitabu kwa watu wote
Huang Kunming, Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mkuu wa Idara ya Uenezi ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, akisoma barua ya pongezi ya Rais Xi Jinping wa China kwenye Mkutano wa Kwanza wa China wa Kusoma Vitabu kwa Watu Wote, na kutoa hotuba katika mkutano huo uliofanyika Beijing, Mji Mkuu wa China, Aprili 23, 2022. (Xinhua/Yan Yan)
BEIJING - Mkutano wa Kwanza wa China wa Kusoma Vitabu kwa Watu Wote ulifanyika hapa Beijing, jana Jumamosi. Rais Xi Jinping wa China, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi, ametuma barua ya pongezi kwa mkutano huo.
“Kusoma vitabu ni njia muhimu kwa watu kupata ujuzi, kupanua hekima, na kuwaandaa kuwa wafuata maadili, kuwapa mwanga na kuwasaidia kuweka malengo ya juu na kurutubisha roho ya ufahari na ukuu. Tangu enzi na dahari, Taifa la China limehimiza kusoma vitabu na kusisitiza upataji wa ujuzi kupitia kujisomea asili ya mambo na kunoa akili kupitia kufikiria kwa usahihi wa maadili. Kusoma vitabu kunasaidia watu wa China kuendeleza moyo wa jadi wa kukua na kujiendeleza bila mwisho, na kutengeneza tabia zao za kujiamini na kujitegemea” Xi ameandika katika barua hiyo.
Ametoa wito kwa wanachama na maafisa wa CPC kuweka kipaumbele katika kusoma vitabu na kujifunza, kukuza maadili na fikra na kuongeza uwezo.
Ameeleza matumaini yake kwamba watoto wote watakuwa na desturi ya kusoma vitabu, kufurahia kusoma vitabu ili kukua vizuri . Pia ameeleza nia yake ya kuona watu wote wa China wakijishiriki katika kusoma vitabu na kuchangia katika mazingira ambayo kila mtu anapenda kusoma vitabu, kusoma vitabu vizuri, na kujua jinsi ya kupata manufaa kutokana na kusoma vitabu.
Huang Kunming, Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Mkuu wa Idara ya Uenezi ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, alisoma barua ya pongezi ya Xi na kutoa hotuba kwenye mkutano huo.
Huang amesema kuwa, barua hiyo inadhihirisha kikamilifu Kamati Kuu ya Chama inatilia maanani sana kuhimiza desturi ya kupenda kusoma vitabu miongoni mwa watu na kujenga mazingira ya watu wote kusoma vitabu nchini China.
Mkutano huo uliandaliwa na Ofisi ya Uchapishaji chini ya Idara ya Uenezi ya Kamati Kuu ya CPC na Idara ya Uenezi ya Kamati ya CPC ya Beijing.
Kaulimbiu ya mkutano huo ni "kusoma vitabu katika zama mpya na kusonga mbele katika safari mpya." Mkutano huo pia umehusisha mfululizo wa mijadala, maonyesho, matukio ya uzinduzi wa vitabu na shughuli kuhusu mada mahsusi.
Maofisa kutoka idara husika pamoja na wajumbe wa wachapishaji, mashirika ya kijamii, wataalamu, wasomi, waandishi na wasomaji walihudhuria kwenye mkutano huo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma