China yaanzisha mradi wa awamu ya nne ya mpango wa utafiti wa mwezi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 26, 2022

BEIJING - Kwa mujibu wa Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Taifa ya Anga ya Juu ya China (CNSA), nchi hiyo itaanza kufanya utafiti na utengenezaji kuhusu mradi wa awamu ya nne ya mpango wake wa utafiti wa mwezi mwaka huu.

Wu Yanhua, Naibu Mkurugenzi wa CNSA, jana Jumapili amesema kwenye hafla ya mtandaoni ya kuanzisha shughuli za Siku ya Anga ya Juu ya China kwa Mwaka 2022 kuwa, vyombo vya Chang'e-6, Chang'e-7 na Chang'e-8 vitarushwa kwa mfululizo kwenye sayari ya mwezi ili kufanya utafiti wa mradi, na nchi ya China itajitahidi kufikia mafanikio katika teknolojia muhimu na kujenga kituo cha kimataifa cha utafiti wa mwezi.

Amesema chombo cha Chang'e-6 kitakwenda kuchukua sampuli kutoka upande wa mbali wa mwezi. CNSA Inapanga kuweka kundinyota la satelaiti kuzunguka mwezi ili kutoa huduma za mawasiliano na uongozi wa usafiri.

“Lengo kuu la mradi wa awamu ya nne ni kufanya utafiti wa kisayansi kwenye ncha ya Kusini ya mwezi na kuanzisha msingi wa kituo cha utafiti wa kisayansi wa mwezi. Awamu ya nne itatekelezwa kwa hatua tatu, na vyombo vya Chang'e-6, Chang'e-7 na Chang'e-8 vitakaofanya utafiti vitarushwa kwenye sayari ya mwezi kabla ya 2030”, amesema Wu.

Katika hafla hiyo, Wu pia alizindua kituo cha ushirikiano wa kimataifa kwa data na matumizi ya satelaiti chini ya CNSA, na kituo cha data na matumizi cha kundinyota la setilaiti za kuhisi kwa mbali cha BRICS (nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini).

Zhang Kejian, Naibu Waziri wa Viwanda na Upashanaji wa Habari ya China, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa , amesema serikali ya China itafuta kanuni za kuwa na usawa na kunufaishana, matumizi ya amani na maendeleo jumuishi, na kufuata dhana ya amani na ushirikiano.

Amesema kuwa serikali ya China itatoa mchango mkubwa zaidi katika utafiti wa Ulimwengu, ustawi wa watu na maendeleo ya ustaarabu wa binadamu, na kufanya kazi na washirika wenzi wa kimataifa kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja katika anga ya juu.

Wakati wa kuadhimisha Siku ya Anga ya Juu ya China kwa Mwaka, zaidi ya shughuli 200 zitafanyika, ikiwa ni pamoja na siku ya kufunguliwa kwa maonesho ya safari kwenye anga ya juu, mihadhara maarufu ya kisayansi, mashindano ya ujuzi, matukio ya mabadilishano na semina.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha