Maonyesho ya Biashara ya Guangzhou, China yavutia idadi kubwa ya wanunuzi wa ng'ambo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 26, 2022

Waonyeshaji wakitambulisha bidhaa kwenye matangazo ya mubashara mtandaoni kwenye banda la Kampuni ya Mavazi ya Guangzhou wakati wa Maonyesho ya Uuzaji na Uagizaji wa bidhaa ya China huko Guangzhou, Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China, Aprili 15, 2022. (Xinhua)

GUANGZHOU-- Maonesho ya 131 ya bidhaa za uuzaji wa nje ya Guangzhou, China yamemalizika hivi punde, maonesho hayo yanajulikana pia kuwa ni Maonesho ya Biashara ya Guangzhou. Idadi ya wanunuzi kutoka nchi na maeneo mbalimbali kwenye maonesho hayo imefikia 536,000 ambayo ni ya rikodi ya juu.

Maonyesho hayo ya biashara yenye hadhi kubwa duniani yalifunguliwa mtandaoni kuanzia Aprili 15 hadi Aprili 24 kwa sababu ya janga la Virusi vya Korona (UVIKO-19).

“Wanunuzi wa ng'ambo waliosajiliwa kwa awamu hiyo ya 131 ya maonyesho waliongezeka kwa asilimia 48 ikilinganishwa na awamu ya 129, na asilimia 41.8 ikilinganishwa na awamu ya 130” anasema Xu Bing, msemaji wa maonyesho hayo.

Xu amesema, miongoni mwao, wanunuzi 298,100 walitoka nchi zilizoshiriki kwenye ujenzi wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, ambazo ni zaidi ya asilimia 55 ya wanunuzi wote, wakati wanunuzi 150,800 walitoka nchi zilizo za wenzi wa ushirikiano wa kiuchumi, ambao ni zaidi ya asilimia 28.

Zaidi ya bidhaa milioni 3 zilionyeshwa mtandaoni, ikijumuisha bidhaa mpya 951,500, hivyo kuweka rekodi mpya. Jukwaa la maonyesho ya mtandaoni lilitembelewa na zaidi ya watu milioni 6.2 katika siku kumi zilizopita. Jumla ya kadi 210,500 za kielektroniki za mawasiliano zilitolewa na waonyeshaji, na takriban mazungumzo 100,000 ya mtandaoni yalifanyika baina ya wanunuzi wa nchi na maeneo mbalimbali .

Takwimu zilionyesha kuwa soko la China bado linaendelea kuvutia watu wengi kutokana na uwezo wake endelevu.

"Licha ya hali ngumu na mbaya ya kiuchumi na kibiashara, mfumo wa Maonyesho ya Biashara ya Guangzhou wa mtandaoni umekuwa thabiti na bora zaidi mwaka huu, ukitoa huduma bora, ambayo imesifiwa sana kwenye maonesho hayo ," Xu amesema.

"Tukio hili limetoa mchango kwa ajili ya kukuza maendeleo ya biashara ya kiwango cha juu, kudumisha uthabiti wa minyororo ya viwanda na ugavi, na kuhimiza ufufukaji wa uchumi wa Dunia," Xu ameongeza.

Tokea Mwaka 1957, maonyesho hayo yamefanyika mara mbili kwa mwaka katika Mji wa Guangzhou, China ili kuhimiza biashara ya Dunia. Na yalifanyika mtandaoni na nje ya mtandao kwa mara ya kwanza katika majira ya mpukutiko mwaka jana.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha