Vikwazo hufanya uchumi wa Dunia kuwa mbaya zaidi: Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 06, 2022

BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian Alhamisi wiki hii amesema kuwa, ukweli tayari umethibitisha kwamba vikwazo haviwezi kuleta amani bali vitafanya uchumi wa Dunia kuwa mbaya zaidi.

Zhao pia amesema kuwa Marekani, ikiwa ni nchi yenye uchumi mkubwa zaidi duniani, inapaswa kufanya mengi zaidi ambayo yanasaidia kufufua uchumi wa Dunia na kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa duniani.

Zhao ameyasema hayo alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu ripoti kwamba Shirika la Fedha Duniani (IMF) hivi karibuni lilishusha makadirio ya ukuaji wa uchumi wa Dunia kwa Mwaka 2022 hadi asilimia 3.6.

Amebainisha kuwa kuimarika kwa uchumi ni matarajio ya pamoja ya watu kutoka nchi zote na kwamba licha ya hali tete na kutokuwa na uhakika, uchumi wa China siku zote umetoa mchango chanya katika uchumi wa Dunia.

Amesema, takwimu za uchumi wa China kwa robo ya kwanza ya Mwaka 2022 zimeonyesha kuwa uchumi wa China umeendelea kuimarika na kasi yake ya maendeleo, na biashara yake ya nje na uwekezaji wa kigeni unaendelea kuimarika, na kuonyesha ustahimilivu na uhai mkubwa.

“China iko tayari kushirikiana na pande zote kuchangia katika kuleta utulivu wa minyororo ya viwanda na ugavi duniani, kuinua uchumi wa Dunia, na kuongeza imani duniani katika maendeleo” msemaji huyo amesema.

Zhao pia amesisitiza kuwa ufufuaji wa uchumi wa Dunia unahitaji juhudi za pamoja za jumuiya ya kimataifa.

“Ikikabiliana na uchumi duni na unaodorora, Marekani na baadhi ya nchi nyingine zinashikilia maslahi yao na kuongeza vikwazo vya upande mmoja kwa upofu” Zhao amesema. Amesisitiza kwamba ukweli tayari umethibitisha kwamba vikwazo haviwezi kuleta amani bali tu vitaufanya uchumi wa Dunia uwe mbaya zaidi, na fimbo kubwa ya vikwazo inawaathiri watu wa nchi zote.

Amesema, Marekani ikiwa ni taifa lenye uchumi mkubwa zaidi duniani, inapaswa kufikiria zaidi haki ya kujikimu na maendeleo ya watu duniani kote, na kufanya juhudi zaidi zinazosaidia kufufua uchumi na utulivu wa minyororo ya ugavi ya Dunia.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha