Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China asema, ni upuuzi kuilaumu China kwa mgogoro wa Russia na Ukraine

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 07, 2022

BEIJING – Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China Le Yucheng Ijumaa wiki hii amesema kwamba shutuma dhidi ya China kuitaka iwajibike kwenye mgogoro wa Ukraine ni upuuzi.

Le aliyasema hayo alipotoa hotuba katika kongamano la mtandaoni la jumuiya za washauri mabingwa wa nchi 20. Kuhusu mgogoro wa Ukraine amesema, baadhi ya watu wanatoa madai yasiyo na msingi, wanapotosha msimamo wa China na kujaribu kuifanya China ilaumiwe kwa matendo yao wenyewe.

Amesema baadhi ya watu wamepindisha maneno ya taarifa ya pamoja ya hivi karibuni ya China na Russia na kutafsiri vibaya maneno ya "urafiki hauna kikomo na ushirikiano hauna maeneo yaliyokatazwa" kumaanisha kwamba China ilikuwa na "ufahamu wa awali" wa operesheni maalum ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine na hata "iliidhinisha" hilo. Kwa hivyo wamehitimisha kuwa China lazima iwajibike kwa mgogoro huo.

"Huu ni upuuzi," Le amesema, akiongeza kuwa China haihusiki katika mgogoro huo, pia si iliyouanzisha. Kwa hivyo China inawezaje kuwajibika?

Le amebainisha kuwa uhusiano kati ya China na Russia unatokana na kanuni za kutofungamana, kutopambana na kutolenga upande wa tatu, na hauko chini ya ushawishi wa upande wa tatu. Maelezo ya "hakuna mipaka" na "hakuna maeneo yaliyokatazwa" yanaonesha hali ya sasa na matarajio ya baadaye ya uhusiano kati ya China na Russia.

“Ukweli ni kwamba, China inataka uhusiano wa kirafiki na nchi zote na kamwe hatuweki kikomo cha ushirikiano” amesema.

Akijibu shutuma kwamba China imesimama katika upande mbaya wa historia kwa kutojiunga na Marekani na nchi nyingine za Magharibi katika kulaani na kuiwekea vikwazo Russia, Le amesema tangu kuzuka kwa mgogoro kati ya Russia na Ukraine, China imekuwa ikishikilia malengo na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kanuni ya usalama usiogawanyika.

"Tumesimamia usawa na haki, na tumefanya juhudi za dhati kuhimiza mazungumzo ya amani na kutoa misaada ya kibinadamu. China haina maslahi binafsi wala haina ajenda yoyote ya siasa za kijiografia kuhusu suala hili," amesema.

Le amesema kwa muda mrefu, Marekani imeendelea kutunisha misuli yake jirani na China, na kuunda vikundi mahsusi dhidi ya China na kuchochea suala la Taiwan ili kujaribu mstari mwekundu wa China.

"Ikiwa hili siyo toleo la upanuzi wa mashariki wa NATO kwenye eneo la Asia-Pasifiki, basi ni nini? Mkakati kama huo, ikiwa hautadhibitiwa, utaleta matokeo ya kutisha na kulisukuma eneo la Asia-Pasifiki kwenye ukingo wa shimo," amesema.

Le amesisitiza kuwa China ina nia ya dhati ya kuleta maendeleo ya amani na inatafuta maelewano, mshikamano na ushirikiano katika eneo hilo. China haijawahi kuwa mchochezi au mkorofi. Haina maana yoyote kuilenga China. Jaribio la "kunakili na kubandika" mgogoro wa Ukraine katika eneo la Asia-Pasifiki linaelekea kushindwa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha