Jumuiya ya Afrika Mashariki yahimiza utayari wa kukabiliana na dharura ya kiafya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 07, 2022

DAR ES SALAAM - Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Ijumaa wiki hii imefanya zoezi la kwanza la kupima utayari tangu kuanza kwa janga la UVIKO-19 ili kuimarisha utayari na kusaidia kukabiliana na dharura za afya ya umma kwa siku zijazo miongoni mwa nchi wanachama.

Taarifa iliyotolewa na makao makuu ya EAC yaliyoko mjini Arusha, Kaskazini mwa Tanzania imesema kuwa zoezi hilo ni sehemu ya warsha ya wiki moja ya mafunzo ya kikanda ili kuimarisha uwezo wa kitaifa wa nchi wanachama wa kuendesha operesheni katika maeneo ya mipakani na bandarini.

Taarifa hiyo imesema zoezi hilo limefanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro nchini Tanzania ili kupima uelewa na ujuzi walioupata washiriki wakati wa warsha ya mafunzo hayo.

“Lengo la zoezi hilo ni kuunganisha tahadhari ya mapema pamoja na utayari na uchukuaji hatua” inasema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema, mbali na janga la UVIKO-19, katika miaka ya hivi karibuni, EAC imekumbwa na milipuko mingi ya magonjwa ya kuambukiza na matukio mengine ya afya ya umma, kama vile ukame na mafuriko.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mlipuko wa janga la UVIKO-19 uliongeza hitaji la kuimarisha uwezo wa kushughulikia dharura za afya ya umma katika maeneo ya bandarini na mipakani.

Nchi wanachama wa EAC ni Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha