China yasema haitasahau shambulio la NATO dhidi ya ubalozi wake mjini Belgrade

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 07, 2022

BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian Ijumaa wiki hii amesema kwamba watu wa China hawatasahau kamwe ukatili wa kinyama wa Jumuiya ya Kujihami ya nchi za Magharibi (NATO) wa kushambulia ubalozi wa China mjini Belgrade Mwaka 1999, na kamwe hawataruhusu maafa hayo ya kihistoria kurudiwa.

Zhao ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akijibu swali linalohusiana na suala hilo, akisema kwamba Mei 7, 1999, NATO inayoongozwa na Marekani ilishambulia kwa bomu ubalozi wa China huko Belgrade, na kuwaua waandishi wa habari watatu wa China na kuwajeruhi wanadiplomasia zaidi ya 20 wa China.

"NATO inadai kuwa jumuiya ya kujihami, lakini kwa kweli mara kwa mara imekuwa ikikiuka sheria za kimataifa na kuendesha vita dhidi ya nchi huru, kudhoofisha amani ya Dunia na kikanda na kuua na kulazimisha idadi kubwa ya watu wasio na hatia kuyakimbia makazi yao ," msemaji huyo amesema.

Amesema NATO inafuata "usalama kamili" na imejihusisha na mawimbi matano mfululizo ya upanuzi wa mashariki baada ya Vita Baridi, ambao haukuifanya Ulaya kuwa salama, lakini imepanda mbegu ya mgogoro kati ya Russia na Ukraine, na kuibua vita katika bara la Ulaya.

“Vita Baridi vimekwisha muda mrefu, na matarajio ya pamoja ya watu kutoka duniani kote ni kukuza amani, ushirikiano na maendeleo”, Zhao amesema.

NATO inayoongozwa na Marekani inapaswa kufanya marekebisho yanayohitajika, kuachana na mawazo ya Vita Baridi, na kuacha kuchochea mapambano ya jumuiya hiyo na kuleta mivutano barani Ulaya, Asia Pasifiki na duniani kote.

“Marekani na NATO zinapaswa kuchukua hatua madhubuti kutoa michango thabiti kwa amani, utulivu na maendeleo ya Dunia”, Zhao ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha