China yazitaka nchi za Kundi la G7 kuacha kuingilia masuala yake ya ndani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 11, 2022

BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Jumanne wiki hii amezitaka baadhi ya nchi za Magharibi ziache mara moja kuingilia masuala ya ndani ya China baada ya Kundi la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa G7 na ofisa mmoja wa Umoja wa Ulaya kueleza wasiwasi wao mkubwa kuhusu uchaguzi wa Ofisa Mkuu wa Hong Kong uliomalizika hivi punde.

John Lee mwenye umri wa miaka 64 ambaye alikuwa mkuu wa ofisi kuu ya mambo ya utawala ya serikali ya Mkoa wa Utawala Maalum wa Hong Kong (HKSAR), Jumapili hii alishinda uchaguzi mkuu wa kwanza tangu kuboreshwa kwa mfumo wa uchaguzi wa mkoa huo Mwaka 2021.

"Nchi na taasisi fulani za Magharibi zinafanya njama za kukashifu uchaguzi na kuingilia mambo ya ndani ya China. China inapinga na kulaani vikali jambo hili," Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian amewaambia waandishi wa habari kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Zhao amesema, baadhi ya nchi zimepuuza ukweli kwamba demokrasia ya Hong Kong imekuwa bora na kwamba maoni mengi ya watu wa Hong Kong yanahitaji umoja na ustawi.

"Wanasikika kama 'wahubiri wa demokrasia' wanaponyooshea vidole uchaguzi wa kidemokrasia wa Hong Kong, kiwango chake cha juu cha kujiamulia mambo yake, na haki za binadamu na uhuru, hali ambayo inafichua tu tabia ya ndumilakuwili na jaribio lao la kuleta machafuko Hong Kong na kuidhibiti China" amesema.

"Hong Kong ni sehemu ya China. Ni aina gani ya mfumo wa uchaguzi ambao Hong Kong inatekeleza na ni aina gani ya njia ya maendeleo ya kidemokrasia inafuata ni masuala ambayo yanaangukia kabisa chini ya wigo wa mambo ya ndani ya China, na hakuna nguvu za nje zilizo na haki ya kuingilia," Zhao amesema.

Amesema Serikali ya China imeazimia kutekeleza kikamilifu na kwa uaminifu kanuni ya "nchi moja, mifumo miwili" na kuendeleza demokrasia ya hali ya juu inayoendana na uhalisia wa mazingira ya Hong Kong, na jaribio lolote la nguvu za nje kudhoofisha hali hii litakuwa bure.

Zhao ameonyesha imani yake kuwa Hong Kong itaanzisha zama mpya ya utawala bora ambao utaleta ustawi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha