Afrika Kusini inahitaji nafasi ya kimaendeleo wakati wa mpito wa nishati: Rais Ramaphosa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 11, 2022

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akitoa hotuba kwenye mkutano wa Uwekezaji katika Indaba ya madini ya Afrika huko Cape Town, Afrika Kusini, Mei 10, 2022. Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Jumanne wiki hii amesema nchi hiyo, kama ilivyo kwa nchi zote zinazoendelea, inapaswa kupewa nafasi ya maendeleo yanayohitajika wakati ambapo iko kwenye mpito wa nishati huku kukiwa na ukosefu wa usalama wa nishati. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)

CAPE TOWN - Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa siku ya Jumanne wiki hii amesema nchi hiyo, kama ilivyo kwa nchi zote zinazoendelea kiuchumi, inabidi ipewe nafasi inayohitajika ya kimaendeleo kwani iko kwenye mpito wa nishati huku kukiwa na uhaba wa nishati.

Ramaphosa ameuambia mkutano wa Uwekezaji katika Indaba ya madini ya Afrika unaofanyika Cape Town kuanzia Jumatatu hadi Alhamisi wiki hii kwamba, wakati ambapo Afrika Kusini inachunguza fursa za mabadiliko ya nishati duniani na kuelekea kwenye madini ya kimkakati ya siku zijazo kama vile shaba, nikeli, cobalt na madini adimu, na vile vile kugeukia madini ya kundi la platinamu na uchumi wa haidrojeni, lazima iendelee kupanua uzalishaji wa madini yake yaliyokwishagunduliwa kwa sasa ambayo yamekuwa "tegemeo" la sekta yake ya madini, ambayo bado ina mahitaji mengi.

Ni muhimu kwamba juhudi za nchi katika kuzalisha kaboni chache ziwe za uhalisia na endelevu, amesema, huku akiongeza kuwa nchi za Afrika "zinahitaji kuwa na uwezo wa kuchunguza na kuchimba mafuta na gesi kwa njia inayowajibika kwa mazingira na endelevu", kwani ni muhimu kwa usalama wa nishati, maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kupunguza umaskini wa nishati.

"Ni muhimu kwamba tunapofanya mabadiliko ya nishati, tuzingatie kanuni zilizomo katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, lakini majukumu tofauti na uwezo husika," amesema, huku akibainisha umuhimu wa kuboresha mazingira ya kazi na maisha ya wafanyakazi wa migodini na jumuiya za wachimbaji madini.

Takwimu rasmi za Serikali ya Afrika Kusini zinaonesha kwamba, sekta ya madini ya nchi hiyo ilirekodi ukuaji wa asilimia 11.8 Mwaka 2021, kiwango cha juu zaidi kuliko sekta zote, na kurejesha uzalishaji kufikia hadi viwango vya kabla ya UVIKO-19 mwaka jana.

Mkutano wa Uwekezaji katika Indaba ya Madini ya Afrika, ambao unaelezwa kuwa mkubwa zaidi katika masuala ya uwekezaji wa madini barani Afrika, unavutia maelfu ya washiriki kutoka serikalini, vikundi vya uchimbaji madini na wahusika lengwa.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akitoa hotuba kwenye Mkutano wa Uwekezaji katika Indaba ya Madini ya Afrika huko Cape Town, Afrika Kusini, Mei 10, 2022. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha