Mtaalamu wa China asema mpunga chotara unachangia usalama wa chakula nchini Burundi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 12, 2022

BUJUMBURA – Mtaalamu wa China Yang Huade ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua siku ya Jumanne wiki hii kwamba, mpunga chotara ambao wataalamu wa kilimo wa China wanakuza nchini Burundi unachangia katika usalama wa chakula wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Yang ambaye alipokea tuzo ya mavuno mazuri “Tuzo ya Balozi wa China nchini Burundi 2022” kutoka kwa Rais wa Burundi mapema mwezi huu, amesema uzalishaji wa mpunga umeongezeka mara tatu tangu alipowasili Burundi Mwaka 2015.

Yang amesema mavuno ya mpunga chotara kwa sasa ni kati ya tani 9 na 10 kwa hekta, ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya Mwaka 2015.

Yang amesema, hapo awali, wakulima wangeweza kuvuna mazao yenye thamani ya takriban faranga 800,000 za Burundi (kama dola 389 za Kimarekani) kwa hekta, lakini kwa sasa faida halisi ni kama faranga milioni 4.8.

"Nilihisi furaha kubwa nilipopokea tuzo kutoka kwa Rais wa Burundi. Hii ilitokana, bila shaka, na kazi nzuri ninayofanya katika sekta ya kilimo ya Burundi", amesema Yang, mkuu wa timu ya wataalam wa kilimo wa China katika Kituo cha Utafiti cha Gihanga nchini humo.

Timu hiyo inaundwa na jumla ya wataalam 13 wakiwemo wataalam 11 kutoka China. Wengine wawili ni raia wa Burundi ambao ni wakaliman.

"Tuliagiza mpunga chotara kutoka China hadi Burundi na mara moja tukapata mavuno mengi ili kuboresha usalama wa chakula nchini Burundi", amesema.

Kwa mujibu wake, kituo hicho kinatoa huduma ya usimamizi kwa vijiji 22 katika majimbo 14 kati ya 18 ya Burundi ambako mpunga unalimwa.

“Kituo hiki kinatoa pembejeo, teknolojia na miongozo kwa wakulima wa mpunga,” amesema.

Kwa mujibu wake, wanafunzi 49 waliopatiwa mafunzo na kituo hicho wanasimamia zaidi ya wakulima 1,500 ambao pia walipata mafunzo ya kilimo cha mpunga katika vijiji hivyo vilivyoko kote nchini.

"Kufanya kazi katika vyama vya ushirika pia ni muhimu kuweka nguvu pamoja. Wakulima wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa taarifa, teknolojia na vifaa. Lakini kupitia vyama vya ushirika, wanaweza kushughulikia matatizo hayo yote", amesema Yang.

Anasisitiza kuwa mbegu za mpunga chotara sasa zinaweza kuzalishwa katika kituo cha utafiti kutokana na msaada wa timu hiyo ya wataalamu.

“Inawezekana kuanzisha kituo cha mbegu na kuzalisha mbegu zenye sifa na hata kuzisafirisha katika mataifa mengine siku za usoni”, amesema Yang.

Mei 2 mwaka huu, katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani katika Jimbo la Muyinga, Kaskazini-Mashariki mwa Burundi, Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye alitoa tuzo kwa wafanyakazi bora na vyama ikiwa ni pamoja na Yang, kwa kufanya "mambo makubwa kwa Burundi" katika kilimo cha mpunga.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha