Wapalestina walaani mauaji ya mwandishi wa habari kwenye Ukingo wa Magharibi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 12, 2022

Wapalestina wakiandamana kupinga mauaji ya mwandishi wa habari wa Al-Jazeera, Shireen Abu Akleh yaliyotkea jana Jumatano asubuhi mjini Jerusalem, Mei 11, 2022. Mauaji ya mwandishi wa habari wa Al-Jazeera Shireen Abu Akleh kwenye Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu na Israel yalizua shutuma na hasira miongoni mwa Wapalestina. (Picha na Muammar Awad/Xinhua)

RAMALLAH/GAZA – Mauaji ya mwandishi wa habari wa Al-Jazeera Shireen Abu Akleh yaliyotokea jana Jumatano asubuhi kwenye Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel yamezua shutuma na hasira miongoni mwa Wapalestina.

Wenzake Abu Akleh, mashahidi wa Kipalestina, na wahudumu wa afya wameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba "wanajeshi wa Israel walimfyatulia risasi yeye na mwandishi mwingine wa habari walipokuwa wakiripoti uvamizi wa Jeshi la Israel kwenye mji wa Jenin, ulioko Kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan."

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotumwa kwa waandishi wa habari, Ofisi ya rais wa Palestina imeitaka Serikali ya Israel kuwajibika kikamilifu kwa kifo cha Abu Akleh.

"Mauaji dhidi ya Abu Akleh ni uhalifu wa kutisha na ni sehemu ya sera ya kila siku inayofuatwa na mamlaka ya Israel dhidi ya Wapalestina, ardhi yao na maeneo yao matakatifu," imesema taarifa hiyo.

Abu Akleh mwenye umri wa miaka 51, Mpalestina-Mmarekani anayeishi Jerusalem Mashariki, amekuwa akifanya kazi na Al-Jazeera kwa zaidi ya miaka 20. Amekuwa akiripoti habari katika maeneo ya Wapalestina, hasa mzozo na mivutano kati ya Israel na Wapalestina.

"Abu Akleh alipigwa kichwani kwa risasi ya Israeli wakati wa uvamizi wa Jeshi la Israeli kwenye kambi ya wakimbizi ya Jenin," Wizara ya Afya ya Palestina imesema katika taarifa.

Iliongeza kuwa Samoudi, mwandishi mwingine wa habari anayefanya kazi Al-Jazeera, alipigwa risasi mgongoni.

Mashuhuda wa Kipalestina wamesema kulikuwa na waandishi wa habari kadhaa wa Palestina waliokuwa wakiripoti uvamizi huo wakati wanajeshi wa Israel walipofyatua risasi.

Shaza Hamaysha, mwandishi wa habari wa Palestina ambaye alisimama karibu na Abu Akleh, ameliambia Xinhua kwamba Shireen "alibaki chini kwa dakika kadhaa, na hakuna mtu aliyeweza kumfikia kutokana na mashambulizi makali ya wanajeshi wa Israel."

Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett amesema kuwa "inaelekea kwamba wapiganaji wa Kipalestina walifyatua risasi kiholela, na wao ndiyo waliosababisha kifo cha bahari mbaya cha mwandishi huyo," kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel.

"Israel imetoa wito kwa Wapalestina kufanya uchunguzi wa maiti na wa pamoja kwa kuzingatia nyaraka na taarifa zilizopo ili kupata ukweli, lakini Wapalestina wanakataa," inasema taarifa rasmi iliyotolewa na ofisi ya Bennett.

Jeshi la Israel lilisema Jumatano kwamba timu maalum ya uchunguzi imeundwa "kuwasilisha ukweli kamili" juu ya mauaji mwandishi huyo.

Hata hivyo Hussein al-Sheikh, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO), alikanusha taarifa ya Bennett. 

Mwanamke wa Palestina akiwa ameshikilia picha ya mwandishi wa habari wa Al-Jazeera Shireen Abu Akleh wakati wa maandamano mjini Jerusalem, Mei 11, 2022. (Picha na Muammar Awad/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha