Uzoefu wa kwanza wa wanafunzi wa Afrika kufanya matangazo ya moja kwa moja ya mauzo ya bidhaa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 12, 2022

Sun Ji (kushoto) akitambulisha pilipili za Rwanda kwa watazamaji katika chumba cha kufanya matangazo ya moja kwa moja. (Picha kwa hisani ya Soko la Gaopiao)

“Yuan 19.9 ni sawa?” “Marafiki, hii ni nafasi yenu!” Katika chumba cha matangazo ya moja kwa moja katika Soko la Gaoqiao, Hunan, waliozungumza Kichina sanifu na kuwasiliana na watazamaji kwa uchangamfu, walikuwa ni wanafunzi Sun Ji kutoka Guinea na Gao Xiang kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Katika Maonesho maalum ya Hunan ya Tamasha la 4 la manunuzi la Shuangpin, yaani Tamasha la Manunuzi ya Bidhaa Nzuri za Afrika la Mtandaoni, wanafunzi hao wawili waafrika walianza uzoefu wao wa kwanza wa kufanya matangazo ya moja kwa moja.

Sun Ji ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili wa kozi ya uchimbaji wa madini katika Chuo Kikuu cha Zhongnan, na amekuwepo nchini China kwa karibu miaka mitatu. Alituambia kuwa ana hamu kubwa kuhusu uuzaji wa bidhaa kwa njia ya video ya kufanya matangazo ya moja kwa moja, mara alipokea mwaliko wa kushiriki kwenye shughuli hiyo alikubali bila kusitasita. Katika chumba cha kufanya matangazo ya moja kwa moja, Sun Ji na mwenzake mchina walitambulisha bidhaa mbalimbali za Afrika: Chai kutoka Kenya, pilipili kutoka Rwanda, kahawa kutoka Ethiopia, korosho kutoka Tanzania na embe kavu kutoka Uganda, kati ya bidhaa hizo, pilipili za Rwanda zilipendwa zaidi na wanunuzi.

Sun Ji alisema: "Pilipili za Rwanda ni tofauti na zile za Hunan. Wachina wengi wanataka kuonja pilipili za Rwanda ili kujua zina tofauti gani na pilipili za Hunan." Pia alisema anahisi urafiki wa Wachina, "Wote walinipongeza kwa kuwa 'ninatambulisha vizuri'."

“Hii ni mara yangu ya kwanza kufanya matangazo ya bidhaa moja kwa moja, mwanzoni nilikuwa na wasiwasi na kuona haya kidogo, lakini baada ya muda mfupi nilizoea." Kuhusu uzoefu huu maalum, Sun Ji alisema anaona heshima sana kushiriki katika shughuli hiyo, ambayo ilikuwa ni shughuli yenye thamani kwake.

Gao Xiang (kulia) akifanya matangazo ya moja kwa moja. (Picha kutoka Soko la Gaopiao)

Gao Xiang, mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Ualimu wa Hunan, ambaye kozi yake ni ufundishaji wa Lugha ya Kichina, na yeye ni mwanafunzi mwingine wa Afrika aliyeshiriki kwenye shughuli hiyo. Katika chumba cha kufanya matangazo ya moja kwa moja ya mauzo ya bidhaa, alivutia mashabiki wengi kwa kichina chake fasaha. Ingawa ni mara yake ya kwanza kushiriki kwenye "matangazo ya moja kwa moja ya mauzo ya bidhaa", hakuwa na woga na alitambulisha bidhaa maalum za nchi yake kwa watazamaji bila tatizo. Alituambia kuwa wote walimuunga mkono sana. "Walisema hawajawahi kuona mwanafunzi wa Afrika akitambulisha bidhaa maalum za Afrika."

Zhang Dan, Mkurugenzi wa Biashara ya Mtandao wa Soko la Gaoqiao la Hunan aliwasifu wanafunzi hao wawili wa Afrika, kuwa ingawa hii ni mara yao ya kwanza kushiriki katika kufanya matangazo ya moja kwa moja ya mauzo ya bidhaa, lakini walifanya vizuri. Aliongeza kuwa si kama tu walileta nyimbo na ngoma za Afrika kwenye chumba cha matangazo hayo, bali pia walitambulisha utamaduni na bidhaa za nchi zao kwa idadi kubwa ya wateja wa China. Soko la Gaoqiao pia litaendelea kutoa jukwaa kwa wanafunzi wa Afrika wanaosoma mkoani Hunan kwa sekta mpya kama matangazo ya moja kwa moja ya mauzo ya bidhaa ili kuhimiza mawasiliano ya utamaduni na biashara kati ya China na Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha