Shirika la Fedha la Afrika (AFC) lazindua mpango wa dola bilioni 2 kusaidia kufufua uchumi wa Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 13, 2022

LAGOS - Shirika la Fedha la Afrika (AFC) limetangaza Alhamisi wiki hii kuwa limezindua mpango wa dola za kimarekani bilioni mbili ili kusaidia kufufua uchumi barani Afrika ulioathiriwa na migogoro ya kimataifa ikiwa ni pamoja na janga la UVIKO-19 na mgogoro wa hivi karibuni zaidi kati ya Russia na Ukraine.

Shirika hilo lenye makao makuu yake nchini Nigeria limesema katika taarifa yake kwamba, limejitolea kutoa fedha hadi kufikia asilimia 50 ya jumla ya gharama za mpango huo na kwamba litahamasisha wadau wengine kupitia mtandao wake wa washirika wa kimataifa na wawekezaji.

Mpango huo utatoa fedha kwenye shirika hilo la kifedha na kuzigawa kwa njia ya mikopo kupitia benki mahususi, benki za maendeleo za kikanda na benki kuu za nchi mbalimbali barani Afrika hivyo kuzipatia ukwasi wa fedha zinazohitajika kugharamia biashara na shughuli nyingine za kiuchumi katika maeneo yao mbalimbali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashirika haya ya kifedha yataboresha ufikiaji wa kifedha wa kimataifa uliothibitishwa na AFC ili kupata mikopo kwa riba za ushindani.

"Janga la UVIKO-19 limerudisha nyuma mwelekeo wa ukuaji wa uchumi wa Afrika na kuongeza zaidi pengo la mitaji ya biashara," Banji Fehintola, Mkuu wa hazina na taasisi za kifedha wa AFC amesema katika taarifa hiyo, huku akiongeza kuwa kabla ya bara hilo kumaliza janga hilo, mgogoro kati ya Russia na Ukraine umeleta changamoto mpya.

"Tumedhamiria kuchukua jukumu kuu katika kuchangiza ufufuaji na ustahimilivu wa kiuchumi wa bara hili, siyo tu kupitia kazi tunayofanya katika kuziba pengo la miundombinu ya Afrika lakini pia kupitia uingiliaji uliolengwa kama vile mpango huu wa dola bilioni mbili za kimarekani kuwezesha uchumi kustahimili janga la UVIKO-19." ameongeza.

Shirika la AFC, lililoundwa na baadhi ya nchi za Afrika Mwaka 2007, lina jukumu la kutoa suluhisho yakinifu juu ya nakisi ya miundombinu ya Afrika na mazingira magumu ya uendeshaji. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha