China yaitaka Marekani kuhimiza amani na utulivu wa kikanda katika mkutano ujao kati yake na ASEAN

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 13, 2022

BEIJING - Marekani, ambayo ni nchi isiyo ya kikanda, inapaswa kuchukua jukumu chanya lenye kujenga katika kukuza amani na maendeleo ya kikanda, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian amesema Alhamisi wiki hii akijibu ripoti kwamba mkutano ujao kati ya Marekani na Nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Asia Kusini Mashariki (ASEAN) utajadili masuala yanayohusiana na China.

"Marekani haipaswi kutumia ushirikiano kama kifuniko ili kulazimisha nchi nyingine kuchagua upande, au kucheza na moto juu ya masuala yanayohusu masilahi makuu ya China," Zhao amesema.

Iliripotiwa kuwa Kurt Campbell, mratibu wa sera za eneo la Bahari ya Hindi na Pasifiki katika Ikulu ya Marekani, White House, amesema kuwa Marekani inatarajia kuchukua hatua za kudumisha amani na utulivu katika Mlango-Bahari wa Taiwan.

Marekani inaendelea kufuata sera ya kuwepo kwa China moja, haiungi mkono "uhuru wa Taiwan," na haina nia ya kuchukua hatua za uchochezi. Lakini "inataka uwazi kuhusu shauku ya kuzuia hatua ambazo zitakuwa za uchochezi," kwa mujibu wa Campbell.

Akijibu kauli hizo, Zhao amesema kanuni ya kuwepo kwa China moja ni makubaliano ya jumuiya ya kimataifa na kanuni ya msingi inayoongoza uhusiano wa kimataifa.

Zhao ameeleza kuwa, Marekani inapaswa kufuata kanuni ya kuwepo kwa China moja na hati tatu za pamoja kati ya China na Marekani, ahadi zake za kisiasa kwa China kuhusu suala la Taiwan, na kauli ya Rais wa Marekani Joe Biden kwamba Marekani haiungi mkono "uhuru wa Taiwan".

“Marekani inapaswa kuacha kutumia masuala yanayohusiana na Taiwan kujihusisha na udanganyifu wa kisiasa katika kujaribu kuidhibiti China” ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha