China na Ethiopia zatazamia kupanua ushirikiano katika uwekezaji na biashara

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 13, 2022

Balozi wa China nchini Ethiopia Zhao Zhiyuan akitoa hotuba wakati wa Kongamano la Ushirikiano kati ya China na Ethiopia katika uwekezaji na biashara mjini Addis Ababa, Ethiopia, Mei 12, 2022. Ethiopia na China Alhamisi wiki hii zimefanya kongamano la ushirikiano katika uwekezaji na biashara ambalo lililenga kupanua biashara na maendeleo baina ya pande hizo mbili. (Xinhua/Wang Ping)

ADDIS ABABA - Ethiopia na China siku ya Alhamisi wiki hii zimefanya kongamano la ushirikiano katika uwekezaji na biashara ambalo lililenga kupanua biashara na maendeleo kati ya pande hizo mbili.

Kongamano hilo limeandaliwa kwa pamoja na Ubalozi wa China nchini Ethiopia, Tume ya Uwekezaji ya Ethiopia (EIC) na Idara ya Uhimizaji wa Uwekezaji ya Wizara ya Biashara ya China huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.

Katika kongamano hilo, pande mbili zilisaini Kumbukumbu za Makubaliano (MOU) kuhusu Ushirikiano katika Uwekezaji kati ya nchi hizo mbili, utakaotumika kama mfumo mpya wa kuhimiza ushirikiano wa uwekezaji na kuleta msukumo kwa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Kongamano hilo lilifanyika katika mfumo wa mseto, limewakutanisha maofisa waandamizi wa serikali ya Ethiopia, mashirika ya wafanyabiashara wa nchi hizo mbili, pamoja na wanadiplomasia wa China mjini Addis Ababa. Maofisa waandamizi wa serikali ya China pia walishiriki kwa njia ya video katika kongamano hilo la ngazi ya juu la uwekezaji na biashara.

Akihutubia kongamano hilo, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Demeke Mekonnen amesisitiza kuwa nchi ya Zambia ya Afrika Mashariki imekuwa miongoni mwa nchi zinazopokea uwekezaji mkubwa wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) barani Afrika, ambapo ushirikiano wa China umeongeza kasi inayohitajika katika kuendesha nchi hiyo.

Amesema uwekezaji wa China katika teknolojia ya mawasiliano, miundombinu mikubwa, maeneo ya viwanda na sekta za utengenezaji wa bidhaa kwa hakika umeongeza juhudi za serikali ya Ethiopia katika kujenga msingi wa maendeleo ya viwanda vyenye nguvu ya ushindani na endelevu.

Naibu Waziri wa Biashara wa China Qian Keming akihutubia kongamano hilo kwa njia ya video, amesisitiza kwamba tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo zaidi ya miaka 50 iliyopita, hali ya kuaminiana kisiasa kati ya nchi hizo mbili imeendelea kuimarika, na ushirikiano katika sekta za uchumi na biashara umepata matokeo ya kivitendo na yenye tija.

"China na Ethiopia zinahitaji kuimarisha mshikamano, kuzidisha urafiki na ushirikiano, kufanya ushirikiano wa kunufaishana na kupata matokeo yenye mafanikio, na kuhimiza maendeleo thabiti katika ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili," alisema.

Alisisitiza kuwa, nchi hizo mbili zinapaswa kutekeleza Miradi Tisa ya ushirikiano kati ya China na Afrika, kuoanisha mikakati ya maendeleo, kuhimiza maendeleo mazuri ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, na kuimarisha utaratibu wa mabadilishano na ushirikiano.

Mwaka 2021, jumla ya thamani ya biashara baina ya nchi hizo mbili ilifikia dola za kimarekani bilioni 2.66, ambapo China iliagiza bidhaa za karibu dola milioni 370 kutoka Ethiopia, ikiwa ongezeko la asilimia 8.1 kwa kulinganishwa na Mwaka 2020.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha