

Lugha Nyingine
Finland na Sweden zaamua rasmi kuomba kujiunga na NATO
Rais wa Finland Sauli Niinisto (kulia) na Waziri Mkuu Sanna Marin wakihudhuria mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Helsinki, Finland, Mei 15, 2022. Rais wa Finland na kamati ya sera ya mambo ya nje ya serikali hiyo jana Jumapili walichukua uamuzi rasmi wa kuanza mchakato wa kuomba nchi hiyo kujiunga na kuwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO). (Xinhua/Chen Jing)
HELSINKI na STOCKHOLM – Finland na Swedeni mwishoni mwa wiki zimetangaza rasmi kuanza michakato ya kujiunga rasmi na Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharigi (NATO).
"Mei 15, Rais na Kamati ya Mawaziri ya Sera ya Mambo ya Nje na Usalama ya Serikali walikamilisha ripoti ya Finland kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi. Ripoti hiyo itawasilishwa kwenye kikao cha mashauriano cha Serikali leo (jana Jumapili)... na baada ya kuidhinishwa, itawasilishwa Bungeni,” imesema taarifa ya Serikali ya Finland.
Akihutubia mkutano na waandishi wa habari pamoja na Waziri Mkuu Sanna Marin, Rais Sauli Niinisto ameitaja siku hiyo kuwa ya kihistoria huku zama mpya ikianza. Amesema kuwa usalama wa Finland siyo wa "kukandamiza nchi nyingine," haulengi nchi yeyote.
Huku pia akiipongeza siku hiyo kuwa ya kihistoria, Marin amesema kufuatia idhini hiyo ya bunge, baraza la mawaziri litapendekeza kwa Rais Niinisto kwamba ombi hilo lipelekwe kwa NATO.
Katika mawasiliano kwa njia simu yaliyofanyika Jumamosi, Niinisto alimfahamisha Rais wa Russia Vladimir Putin kuhusu uamuzi wa Finland wa kutafuta uanachama wa NATO katika siku chache zijazo. Kremlin ilisema katika taarifa yake kwamba "Putin amesisitiza kwamba kuacha sera ya jadi ya kutoegemea upande wowote kijeshi itakuwa kosa, kwani hakuna vitisho kwa usalama wa Finland."
Wakati huohuo, huko Stockholm Sweden, Chama Tawala cha Social Democratic (SAP) jana Jumapili kimekubali na kuunga mkono ombi la nchi hiyo kujiunga na kuwa mwanachama wa NATO, ikiwa ni kuashiria mabadiliko ya kimsingi ya msimamo wa chama hicho ambacho kilikuwa mpinzani mkubwa wa NATO.
"Sisi Social Democrats tunaamini kwamba jambo bora zaidi kwa usalama wa Sweden ni kwamba tunajiunga na NATO," Waziri Mkuu wa Sweden Magdalena Andersson, ambaye pia ni kiongozi wa SAP, alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Stockholm baada ya mkutano wa chama hicho.
Rais wa Finland Sauli Niinisto (kulia) na Waziri Mkuu Sanna Marin wakihudhuria mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Helsinki, Finland, Mei 15, 2022. (Xinhua/Chen Jing)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma