Takriban raia 100, wengi wao wakiwa walioyakimbia makazi yao wauawa Mashariki mwa DRC

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 18, 2022

UMOJA WA MATAIFA - Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric Jumanne wiki hii amesema kuwa, mauaji ya takriban raia 100 Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wiki iliyopita yanaibua wasiwasi juu ya kuendelea kukosekana kwa usalama katika eneo hilo.

Stephane Dujarric, amesema mashirika ya kibinadamu nchini DRC yameonyesha wasiwasi wao baada ya msururu wa mashambulizi mabaya, hasa kwenye maeneo ya watu waliokimbia makazi yao. Mashambulizi hayo yanakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.

"Tangu mapema wiki iliyopita, karibu raia 100 wameuawa katika mfululizo wa mashambulizi katika jimbo la Ituri," Dujarric amesema. "Wanawake na watoto ni miongoni mwa waathiriwa."

Amesema zaidi ya raia 500 waliripotiwa kuuawa tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Takriban mashambulizi 12 dhidi ya shule na hospitali pia yaliripotiwa.

Msemaji huyo amesema mashambulizi ya mwezi mmoja uliopita yamewalazimu zaidi ya watu 165,000 kuyakimbia makazi yao katika eneo la Djugu. Ukosefu wa usalama pia huathiri ufikiaji wa huduma za kibinadamu, kuzuia operesheni za timu za kibinadamu na kuchelewesha usambazaji wa misaada.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha