

Lugha Nyingine
China yasema uchumi wake utarejea kwenye hali ya kawaida hivi karibuni
BEIJING - Meng Wei, Msemaji wa Kamati ya Taifa ya Maendeleo na Mageuzi ya China (NDRC) Jumanne wiki hii amesema, uchumi wa nchi hiyo utarejea katika shughuli zake za kawaida hivi karibuni kutokana na udhibiti madhubuti wa janga la virusi vya Korona na sera husika zinazotekelezwa.
“Uchumi sasa unakabiliwa na upepo mkali kutokana na athari zisizotarajiwa zinazohusiana na kuibuka tena kwa maambukizi ya virusi vya Korona na msukosuko wa hali ya Dunia” Meng amesema katika mkutano na waandishi wa habari.
“Hata hivyo, ikumbukwe kuwa Mwaka 2020 wakati mlipuko wa ghafla wa UVIKO-19 ulipoleta pigo ambalo halijawahi kushuhudiwa, China iliweza kubadilisha haraka kushuka kwa baadhi ya viashiria vya uchumi kupitia udhibiti thabiti wa janga na kushuhudia kufufuka upya kwa uchumi robo baada ya robo ya mwaka” amesema Meng.
Meng amesema NDRC itaongeza marekebisho ya sera za jumla na kusaidia makampuni kurejesha uwezo wa uzalishaji.
NDRC inalenga utekelezaji bora wa sera na kupata matokeo madhubuti katika nusu ya kwanza ya mwaka, Meng amesema, huku akiongeza kuwa pia itabuni zana za sera za nyongeza ili kusaidia kuufanya uchumu ukue kwa hatua madhubuti .
“Licha ya janga hilo na hali ngumu na kali ya kimataifa, China ina uwezo na ujasiri wa kudumisha bei thabiti” Meng amesema.
Ameongeza kuwa NDRC haitaacha juhudi zozote katika kuhakikisha ugavi wa bidhaa ikiwa ni pamoja na nafaka, makaa ya mawe na madini huku ikiimarisha udhibiti dhidi ya vitendo vya kubahatisha.
Akizungumzia wasiwasi juu ya uendeshaji wa biashara na matarajio ya makampuni ya kigeni nchini China, Meng amesema China bado ni nchi inayovutia zaidi uwekezaji wa kigeni na faida zake za mfumo kamili wa viwanda, miundombinu na soko kubwa zaidi.
“NDRC inafanya jitihada kupanua orodha ya viwanda vinavyohimiza uwekezaji wa kigeni, kwa kuzingatia viwanda na huduma za uzalishaji na kuelekeza uwekezaji zaidi katika maeneo ya Kati, Magharibi na Kaskazini Mashariki mwa China,” Meng amesema.
Takwimu rasmi zilionyesha kuwa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni katika China Bara, katika matumizi halisi, uliongezeka kwa asilimia 26.1 kuliko mwaka uliopita hadi dola za kimarekani bilioni 74.47 katika miezi minne ya kwanza ya Mwaka 2022, kwa msingi wa ukuaji wa asilimia 38.6 katika kipindi kama hicho mwaka jana.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma