Rais Xi Jinping asisitiza nia ya China ya kufungua mlango kwa kiwango cha juu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 19, 2022

Rais Xi Jinping wa China akihutubia kwa njia ya video kwenye Mkutano wa maadhimisho ya miaka 70 ya Kamati ya Uhimizaji wa Biashara ya China na Mkutano wa Kuhimiza Biashara na Uwekezaji wa Kimataifa, Mei 18, 2022. (Xinhua/Li Xueren)

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping Jumatano wiki hii amesisitiza kwamba nia ya China ya kufungua mlango kwa kiwango cha juu haitabadilika, na mlango wa China utafunguliwa zaidi kwa Dunia.

Xi aliyasema hayo wakati akihutubia kwa njia ya video mkutano wa maadhimisho ya miaka 70 ya Kamati ya Uhimizaji wa Biashara ya China (CCPIT) na Mkutano wa Kuhimiza Biashara na Uwekezaji wa Kimataifa.

Akidhihirisha kwamba, tangu kuanzishwa kwa Kamati ya Uhimizaji wa Biashara ya China Mwaka 1952, kamati hiyo inajikita katika kazi yake ya nchini China huku ikielekea dunia, imeonesha umuhimu wake katika kuimarisha maslahi kati ya wafanyabiashara wa China na wa nje , kuhimiza mawasiliano ya kimataifa katika uchumi na biashara, na kusukuma mbele maendeleo ya uhusiano baina ya nchi.

Xi amesisitiza kuwa Dunia inakabiliwa na janga na mabadiliko makubwa ambayo hayajapata kuonekana katika karne moja, utandawazi wa kiuchumi unakabiliwa na upepo mkali, na dunia inaingia katika kipindi kipya cha msukosuko na mabadiliko. Amesema, sasa kuliko wakati mwingine wowote, wafanyabiashara duniani kote wanatamani amani na maendeleo, kutoa wito wa usawa na haki, na kutamani ushirikiano wa kunufaishana.

Amesisitiza juu ya kuweka kipaumbele kwa watu na maisha yao, kushiriki kikamilifu katika ushirikiano wa kimataifa juu ya utafiti na maendeleo, uzalishaji na usambazaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19, kuimarisha usimamizi wa afya ya umma duniani, kujenga kwa pamoja njia nyingi za kujikinga na virusi, na kuhimiza kujenga jumuiya ya afya ya binadamu.

Xi pia amesisitiza haja ya kuendeleza Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030 ya Maendeleo Endelevu katika nyanja zote, na kusaidia uchumi wa Dunia kuboresha vichocheo vya ukuaji wake, kurekebisha muundo wake wa ukuaji ili kuuelekeza vizuri kwenye njia ya muda mrefu, na ukuaji thabiti.

Ili kuwezesha mafanikio ya maendeleo ya kiuchumi kuwafikia watu wa nchi zote, Xi amehimiza kuunga mkono mfumo wa biashara wa pande nyingi chini ya kiini cha WTO, kuhakikisha usalama na utulivu wa minyororo ya viwanda na ugavi duniani, na kupanua ushirikiano ili kuleta manufaa kwa nchi na watu.

Xi amesisitiza juhudi za kuzidisha mabadilishano na ushirikiano katika uvumbuzi, kuhimiza mafungamano ya maendeleo ya sayansi na teknolojia na ukuaji wa uchumi, kuongeza mgawanyo wa matokeo ya uvumbuzi, na kuondoa vikwazo vyote vinavyozuia mtiririko wa maarifa, teknolojia, vipaji na mambo mengine ya uvumbuzi.

Xi amesisitiza kwamba "Nia ya China ya kufungua mlango kwa kiwango cha juu haitabadilika, na kwamba mlango wa China utafunguliwa zaidi kwa dunia " .

Amesema kwamba, China itaendelea kuhimiza mazingira ya biashara yanayofuata kanuni za soko, zinazosimamiwa kwa sheria na kufikia viwango vya kimataifa. 

Rais Xi Jinping wa China akihutubia kwa njia ya video kwenye Mkutano wa maadhimisho ya miaka 70 ya Kamati ya Uhimizaji wa Biashara ya China na Mkutano wa Kuhimiza Biashara na Uwekezaji wa Kimataifa, Mei 18, 2022. (Xinhua/Yin Bogu)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha