Tanzania yaandaa kongamano la kuadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Nyerere

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 19, 2022

Chen Mingjian, Balozi wa China nchini Tanzania, akizungumza kwenye kongamano la kuadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam, Tanzania, Mei 17, 2022. Kongamano hilo la siku moja limefanyika Jumanne wiki hii jijini Dar es Salaam, limeandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na Ubalozi wa China nchini Tanzania. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)

DAR ES SALAAM - Kongamano la siku moja la kuadhimisha miaka mia moja tangu kuzaliwa kwa Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere limefanyika Jumanne wiki hii jijini Dar es Salaam, mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania.

Kongamano hilo limeandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na Ubalozi wa China nchini Tanzania.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema Nyerere anapaswa kukumbukwa kwa kuwa mtu mwenye misimamo na imani ya hali ya juu.

"Aliamini katika ubinadamu, haki za binadamu, na haki za watu binafsi na jamii. Aliamini katika amani na umoja," amesema Butiku.

Chen Mingjian, Balozi wa China nchini Tanzania, amesema Nyerere aliweka msingi wa urafiki wa kina na thabiti kati ya China na Tanzania, na kuleta jadi ya kushirikiana katika mafanikio na changamoto kati ya nchi hizo mbili.

“Rais Nyerere alijitolea kukuza urafiki kati ya China na Tanzania katika maisha yake yote, huku akiacha hadithi nyingi,” Chen amesema kwenye Kongamano hilo lililohudhuriwa na viongozi wastaafu wa Tanzania, viongozi wa vyama vya siasa, mabalozi na makamishna wakuu wa nchi za nje nchini Tanzania, na wawakilishi wa wataalamu washauri, mashirika ya hisani na vyombo vya habari.

Deng Li, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China, alitoa ujumbe kwa njia ya video, akisema Nyerere alipendwa sana na watu wa Tanzania, alipata heshima kubwa barani Afrika, na anajulikana na kuheshimiwa na watu wa China.

“Tunamkumbuka Rais Nyerere ili kuendeleza urithi wake wa ujasiri na ushujaa, kurejea historia ya urafiki, mshikamano na ushirikiano kati ya China na Tanzania na China na Afrika na kutengeneza mwelekeo wa mustakabali wa uhusiano kati ya China na Tanzania na China na Afrika," amesema Deng.

Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hamza Hassan Juma, amesema Nyerere na Kiongozi Mwasisi wa Zanzibar, Abeid Amani Karume ndiyo waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioanzishwa Mwaka 1964 hadi kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Juma ameongeza kuwa Nyerere alisisitiza umuhimu wa kukuza utamaduni wa Mwafrika katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Mkurugenzi wa Kituo cha Masomo kuhusu China cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey Moshi, amesema katika miongo miwili iliyopita, China imekuwa mshirika mwenzi muhimu zaidi wa kiuchumi wa Afrika katika masuala ya biashara, uwekezaji na ujenzi wa miundombinu.

Moshi amesema ushirikiano kati ya Afrika na China ikiwamo Tanzania umewezesha uchumi wa Afrika kupitia biashara, uwekezaji na misaada ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini na kusukuma mbele maendeleo ya viwanda.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku akizungumza kwenye kongamano la kuadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam, Tanzania Mei 17, 2022. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha