Jukwaa la Uchumi Duniani kukabiliana na changamoto za kijiografia za kiuchumi huko Davos

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 19, 2022

GENEVA – Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) limetangaza Jumatano wiki hii kwamba Mkutano wake wa Mwaka 2022 utaangazia changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa duniani ambazo serikali zinakabiliana nazo hivi sasa, ikiwa ni pamoja na kufufuka kwa uchumi baada ya janga la UVIKO-19, mgogoro wa Ukraine na mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano huo, unaoitwa "Historia Katika Hatua ya Mabadiliko: Sera za Serikali na Mikakati ya Kibiashara," utafanyika Davos, Uswizi, Mei 22-26.

“Baada ya kusimama kwa miaka miwili kwa sababu ya janga la UVIKO-19, ikifuatiwa na mgogoro wa Ukraine na changamoto zingine za uchumi kijiografia, mkutano unafanyika katika wakati muhimu” WEF imesema.

Mkutano huo unatazamiwa kuwakutanisha pamoja viongozi na wataalamu karibu 2,500 kutoka kote duniani, kwa nia ya "kuunganisha tena, kubadilishana maarifa, kupata mitazamo mipya na suluhisho za mapema."

"Mkutano wa Mwaka ni mkutano wa kwanza wa kilele unaowakutanisha kwa pamoja viongozi wa Dunia katika hali hii mpya ya Dunia kuwa na usawa wa nguvu miongoni mwa nchi hususani zile kubwa kutokana na janga la UVIKO-19 na vita," amesema Klaus Schwab, mwanzilishi na mwenyekiti mtendaji wa WEF.

"Ukweli kwamba karibu viongozi 2,500 kutoka kwenye nyanja za siasa, mashirika ya kiraia ya kibiashara na vyombo vya habari wanakutana ana kwa ana inaonyesha hitaji la jukwaa la kimataifa linaloaminika, lisilo rasmi na lenye mwelekeo wa kuchukua hatua kukabiliana na masuala katika Dunia inayoongozwa na mgogoro."

“Zaidi ya wakuu wa nchi na serikali wapatao 50 wanatarajiwa kushiriki” WEF imesema. Zaidi ya viongozi 1,250 kutoka sekta ya kibinafsi pia watashiriki, pamoja na "Wavumbuzi wa Kimataifa" na "Waanzilishi wa Teknolojia." wanaofikia 100.

WEF imesema, ajenda ya mkutano huo itazingatia mada sita, ikijumuisha: kukuza ushirikiano wa kimataifa na kikanda; kufanikisha kufufuka kwa uchumi na kutengeneza zama mpya ya ukuaji; kujenga jamii zenye afya na usawa; kulinda tabianchi, chakula na mazingira ya asili; kuendesha mageuzi ya sekta ya viwanda; na kutumia nguvu ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.

Wafanyabiashara maarufu duniani na viongozi wa serikali za nchi mbalimbali wanahitaji kushirikiana kwa pamoja ili kuendeleza sera na mikakati ya muda mrefu ya kufufua uchumi wa Dunia ulioathirika vibaya, kuinua maendeleo ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, na kukabiliana na tishio kubwa zaidi kwa binadamu, mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano huu unafanyika wakati ambao Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeonya katika mtazamo wake wa Uchumi wa Dunia Mwezi uliotolewa Aprili mwaka huu kwamba ukuaji wa uchumi wa Dunia unatarajiwa kupungua kutoka wastani wa asilimia 6.1 Mwaka 2021 hadi asilimia 3.6 Mwaka 2022 na 2023.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha