Rais Xi Jinping atoa wito kwa nchi za BRICS kujenga jumuiya ya kimataifa yenye usalama kwa wote

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 20, 2022

Rais Xi Jinping wa China akitoa hotuba kwa njia ya video kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ushirikiano wa Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini (BRICS), Mei 19, 2022. (Xinhua/Li Xueren)

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping siku ya Alhamisi wiki hii ametoa wito kwa nchi za Ushirikiano wa Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini (BRICS) kushirikiana kwa pamoja ili kujenga jumuiya ya usalama wa dunia nzima.

Xi aliyasema hayo alipotoa hotuba kwa njia ya video kwenye ufunguzi wa mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa BRICS.

Xi alieleza kuwa, hivi sasa athari za mabadiliko makubwa na janga la UVIKO-19 ambalo halijapata kuonekana katika karne moja iliyopita zimeunganishwa, na sababu za kuleta hali isiyo ya utulivu, isiyo na uhakika na isiyo ya usalama zinaongezeka katika hali ya kimataifa.

"Pamoja na hayo, amani na maendeleo bado ni mada isiyobadilika ya nyakati, matarajio ya watu katika nchi mbalimbali kwa ajili ya maisha bora bado hayajabadilika, na majukumu ya kihistoria ya jumuiya ya kimataifa kufuata mshikamano na ushirikiano, na kufanya ushirikiano wa kunufaishana ili kupata maendeleo kwa pamoja bado hayajabadilika," Xi amesema.

Nchi za BRICS zikiwa ni nguvu yenye hamasa, yenye msukumo na ya kiujenzi kwenye jumuiya ya kimataifa, zinapaswa kuimarisha imani, kustahimili dhoruba na mawimbi, na kuchukua hatua za kweli ili kukuza amani na maendeleo, kulinda usawa na haki, na kutetea demokrasia na uhuru, ili kuingiza utulivu na msukumo kwenye uhusiano wa kimataifa katika kipindi cha misukosuko na mabadiliko.

Rais Xi amesisitiza kwamba historia na hali halisi ilivyo zinatuambia kwamba kutafuta usalama wa nchi kwa gharama ya nchi nyingine kutaleta tu mivutano na hatari mpya. Ili kuhimiza usalama wa pamoja duniani, Xi alitoa Pendekezo la Usalama wa Dunia Nzima siku chache zilizopita:

“Nchi za BRICS zinapaswa kuimarisha hali ya kuaminiana kisiasa na ushirikiano wa kiusalama, kudumisha mawasiliano na uratibu wa karibu katika masuala makubwa ya kimataifa na ya kikanda, kushughulikia maslahi ya msingi ya kila upande na ufuatiliaji wao kuhusu masuala makuu, kuheshimu mamlaka ya nchi, usalama na maslahi ya maendeleo ya kila upande, kupinga umwamba na siasa za mabavu, kukataa Mtazamo wa Vita Baridi na makabiliano ya kambi, na kujenga kwa pamoja jumuiya ya kimataifa ya usalama wa dunia nzima ”.

Maendeleo ni kazi ya pamoja kwa nchi zenye masoko yanayoibuka na nchi zinazoendelea, Xi amesisitiza, huku akiongeza kuwa kukabiliana na hatari na changamoto mbalimbali za sasa, ni muhimu zaidi kwa masoko yanayoibuka na nchi zinazoendelea kuimarisha mshikamano na ushirikiano.

Ametoa wito kwa nchi hizo tano za BRICS kushiriki katika mazungumzo na mabadilishano na nchi nyingi zaidi zenye masoko yanayoibuka na nchi zinazoendelea ili kuongeza maelewano na kuaminiana, kuimarisha uhusiano wa ushirikiano, kuzidisha muunganiko wa maslahi, ili kupanua ushirikiano kuwa mkubwa zaidi na nguvu ya maendeleo kuwa imara zaidi, na kuchangia zaidi katika kutimiza matumaini ya kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.  

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha