Tanzania yavuka lengo la Chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio kwa watoto

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 02, 2022

DAR ES SALAAM - WAZIRI wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu jana Jumatano ameielezea kampeni ya nchi hiyo ya utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kuwa yenye mafanikio makubwa.

Ummy amesema watoto milioni 12.1 wenye umri chini ya miaka mitano walipatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa huo kati ya Mei 18 na Mei 21 kwa Tanzania Bara na Zanzibar ikiwa ni zaidi ya lengo lake la awali la kuchanja watoto 10,313,887.

“Haya ni mafanikio makubwa,” Mwalimu amesema kwenye mkutano na wanahabari uliofanyika Dodoma, Mji Mkuu wa Tanzania.

Amesema kampeni nyingine ya chanjo dhidi ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano itafanyika Julai na Agosti mwaka huu kwa tarehe zitakazotangazwa baadaye na kuwataka watu kuwachanja watoto wao kwa wingi.

Awamu ya kwanza ya kampeni ya chanjo hiyo ilifanyika Machi 24 hadi Machi 27 na kuwafikia watoto zaidi ya milioni moja katika mikoa minne ya Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe inayopakana na Malawi baada ya nchi hiyo kuripoti mlipuko wa virusi hivyo.

Malawi ilitangaza mlipuko wa virusi vya polio Tarehe 17, Februari mwaka huu baada ya kisa kugunduliwa kwa mtoto mdogo.

Tanzania ilithibitishwa kuwa haina ugonjwa wa polio Mwaka 2015, baada ya miaka mingi kupita bila kuwa na maambukizi mapya, licha ya mfumo madhubuti wa ufuatiliaji, imesema taarifa hiyo na kuongeza kuwa kutokana na kuwa na mwendelezo wa kiwango cha juu cha kutoa chanjo za kumeza, Tanzania haijaripoti kuwa na mgonjwa wa polio tangu Mwaka 1996.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha