Tanzania yazindua mpango kabambe wa uhifadhi wa mazingira wakati wa kuadhimisha siku ya mazingira duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 06, 2022

DAR ES SALAAM - Tanzania jana Jumapili imezindua mpango kabambe wa uhifadhi wa mazingira ikiwa ni sehemu ya matukio ya kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.

Mpango huo umezinduliwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaliwa mjini Dodoma na kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ya Tanzania kutenga bajeti ya utekelezaji wake katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

“Mpango huo unalenga kurejesha maeneo yaliyoharibiwa na wakati huo huo kudhibiti uharibifu zaidi wa mazingira”, Majaliwa amesema.

Amezitaka wizara na taasisi za serikali, sekta binafsi na watu binafsi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mpango huo ambao amesema umezingatia ulinzi na uhifadhi katika maeneo 15, ikiwemo upandaji miti mingi, udhibiti wa mimea vamizi katika maeneo ya hifadhi, uhamasishaji wa matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, na kudhibiti milipuko ya moto kwenye misitu.

“Maeneo mengine ni ulinzi wa vyanzo vya maji, ulinzi wa korido za wanyama dhidi ya kuvamiwa na shughuli za binadamu, udhibiti wa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori na utengenezaji wa mifumo kamili ya udhibiti wa taka” Majaliwa amesema.

Zlatan Milisic, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, ameipongeza Tanzania kwa juhudi za kuhifadhi mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tanzania imedhihirisha kuwa mshirika mwenzi wa kuaminika katika uhifadhi wa mazingira,” amesema.

Siku ya Mazingira Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Juni 5, ni njia kuu ya Umoja wa Mataifa ya kuhimiza uhamasishaji na hatua za kulinda mazingira.

Ikiwa iliadhimishwa kwa mara ya kwanza Mwaka 1973, siku hiyo imekuwa jukwaa la kuongeza uelewa juu ya masuala ya mazingira kama vile uchafuzi wa mazingira ya baharini, ongezeko la watu, ongezeko la joto duniani, matumizi endelevu na uhalifu dhidi ya wanyamapori.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha