Urushaji wa Chombo cha Shenzhou-14 cha China kwenye anga ya juu wavutia hisia duniani kote

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 07, 2022

Picha iliyopigwa Juni 5, 2022 kwenye skrini katika Kituo cha Udhibiti wa Anga cha Beijing ikionyesha wanaanga watatu wa China, Chen Dong (katikati), Liu Yang (Kulia) na Cai Xuzhe, wakitoa salamu baada ya kuingia kwenye moduli ya msingi ya kituo cha anga za juu cha Tianhe. (Xinhua/Li Xin)

BEIJING - Urushaji wenye mafanikio wa Chombo cha Shenzhou-14 cha China kwenye anga ya juu umeripotiwa na vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa huku waangalizi wa kimataifa wakiuelezea kuwa ni hatua mpya katika juhudi za China kukamilisha kituo chake cha anga za juu na kuchunguza anga.

Siku ya Jumapili, wanaanga watatu wa China waliokuwa kwenye chombo cha anga za juu cha Shenzhou-14 walitumwa angani na kuingia kwenye moduli ya msingi ya kituo cha anga za juu cha Tianhe. Huu ni ujumbe wa 23 wa safari za roketi tangu kuidhinishwa na kuzinduliwa kwa mpango wa anga za juu wa nchi hiyo na ujumbe wa tatu wa wafanyakazi wa mradi wa kituo cha anga za juu cha China.

“Kuruka kwa chombo cha anga za juu cha Shenzhou-14 hadi kwenye kituo cha anga cha Tiangong kumeonyesha mwanzo wa muongo ambapo wanaanga wa China wataendelea kuishi na kufanya kazi katika mzunguko wa chini wa Dunia”, Shirika la Habari la Russia la Regnum limeripoti.

Gazeti la Moscow Komsomolets limeeleza kwa kina mipango ya China ya kujenga kituo cha anga za juu cha Tiangong.

Huku likidhihirisha kuwa China imefanikiwa kutuma timu nyingine ya wanaanga angani ili kukamilisha kituo chake cha anga za juu, Shirika la Habari la Ujerumani, DPA limeripoti kuwa kituo cha anga za juu kinasisitiza matarajio ya China ya kuyafikia mataifa makubwa yenye programu za kurusha roketi na wanaanga kwenye anga za juu.

“Mpango wa anga ya juu wa China tayari umepata mafanikio kadhaa”, limeongeza.

Mnajimu kutoka Croatia Ante Radonic amesema katika mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba urushaji huo wenye mafanikio wa chombo unaonyesha kwamba teknolojia ya China ya anga ya juu imepevuka na kila kitu kinakwenda kwa mujibu wa ratiba.

“Ujenzi wa kituo cha anga za juu cha China utakamilika hivi karibuni”, mwanaastronomia huyo amesema.

Akiweka bayana kuwa China ni nchi ya tatu duniani yenye uwezo wa kufanya shughuli za anga za juu kwa kujitegemea, Radonic amesema kwamba mpango wa China wa kurusha roketi na wanaanga kwenye anga ya juu tayari una nafasi ya kwanza duniani, na programu ya kituo cha anga ya juu inaonyesha zaidi maendeleo ya kasi ya teknolojia ya China ya anga ya juu.

Vyombo vya habari vikuu vya Korea Kusini, ikiwa ni pamoja na shirika la habari la Yonhap na KBS, pia vimeripoti kuhusu urushaji huo.

Kituo cha anga za juu cha China kimevutia hisia za watu wengi, shirika la habari la Yonhap limeripoti, na kuongeza kuwa ikiwa Kituo cha Kimataifa cha Anga za juu kitakamilika na kuzinduliwa, kituo cha anga cha Tiangong cha China kitakuwa kituo pekee cha anga za juu ulimwenguni. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha